Ardhi Dodoma yageuka lulu watu lukuki waisaka

Muktasari:

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Pascas Mulagiri amesema watapima ardhi ya kutosha ili kuziwezesha wizara, taasisi, watumishi na watu watakaohamia mjini hapa kupata viwanja.

Dodoma. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Pascas Mulagiri amesema watapima ardhi ya kutosha ili kuziwezesha wizara, taasisi, watumishi na watu watakaohamia mjini hapa kupata viwanja.

Hali hiyo imekuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kutangaza Serikali kuhamia mjini hapa.

Akizungumza mjini hapa jana, Mulagira alisema kufuatia kauli hiyo ya Rais, wizara, watumishi wa umma na taasisi za Serikali zimewasilisha maombi ya kutaka kugawiwa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi zao.

 “Kumekuwa na ongezeko kubwa la maombi ya wizara, taasisi za Serikali na idadi kubwa ya watumishi wa umma wanaomba kupatiwa viwanja,” alisema.

Alisema katika kuwezesha azma hiyo ya Serikali, ofisi yake ina mpango wa mpito wa kupata makazi na kuhamasisha watu wenye nyumba mjini hapa, kuzipangisha kwa watumishi wa umma watakaohamia Dodoma.

Mulagiri alisema wameunda kamati maalumu inayoratibiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ili kukamilisha azma hiyo.