Ardhi yawachonganisha CCM, wateule na wanasiasa

Muktasari:

Kamati ya siasa kukutana wiki hii kulijadili

Kibaha Vijijini. Chama cha Mapinduzi (CCM ) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kimetishia kuwashtaki kwa mwenyekiti wake Taifa, Rais John Magufuli baadhi ya madiwani na mwenyekiti wao, mbunge na mkuu wa wilaya kwa madai ya kushindwa kusimamia ilani ya chama hicho eneo la ardhi.

Akizungumza kwenye kikao cha bajeti ya 2018/19 cha Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini, Murtala Mkumba alisema chama kimesikitishwa na hatua ya halmashauri kushindwa kuwapimia wananchi maeneo yao katika kata ya Kikongo, huku Rais Magufuli alishtoa agizo hilo mwaka mmoja uliopita.

Mkumba alibainisha kuwa hata kwenye makadirio ya bajeti ya mwaka 2018/19, halmashauri hiyo haijatenga fedha kwa ajili upimaji katika eneo hilo lenye eka 500 ambalo Rais Magufuli mwishoni mwa mwaka juzi alilirudisha na kuelekeza wapatiwe wananchi kwa shughuli za kilimo.

“Baba wa Taifa alisema ili tuendelee tunahitaji mambo manne; ardhi, watu, siasa safi na utawala bora lakini kama chama nasikitika sana suala la ardhi tunacheza nalo, haiwezekani rais anatoa maelekezo halafu sisi tunatengua kauli yake, ni aibu hata bajeti ya kupima eneo hili hamjatenga” alisema Mkumba na kuongeza: “Cha kushangaza mnasema hamjawagawia wananchi kwa sababu hakuna fedha za upimaji, ninazo taarifa wapo wawekezaji mmewapimia na mmoja nahifadhi jina mmempimia tayari eka 1,000, mmemuuzia kwa Sh1 milioni kila eka. Mnadhani sijui, nashangaa tu fedha za kumpimia huyu mnazo ila wananchi hakuna.”

Alimuagiza mwenyekiti wa halmashaurim Mansour Kisebengo, mbunge Hamoud Jumaa, mkuu wa wilaya, Assumpter Mshama na mkurugenzi kukutana mara moja wiki hii na kamati ya siasa kujadili jambo hilo.

Naye Jumaa alisema kuwapo kwa kikao cha kamati ya siasa cha kujadili eneo hilo ni uamuzi sahihi, kwa kuwa hawezi kupingana na chama wala Rais, anachojua ni kusimamia ilani kwa kuhakikisha wananchi hawaonewi.

Akizungumzia suala hilo, Mshama alikiri kuwapo ucheleweshaji upimaji eneo hilo kwa ajili ya wananchi na kwamba, hayupo tayari kupingana na kauli ya Rais kwani hatua ya kuuzwa ardhi kwa Sh1 milioni ni kama imetolewa bure.