Arsenal kuibeba Rwanda katika utalii

Muktasari:

Katika mkataba huo wa miaka mitatu nembo ya Rwanda itaonekana kwenye jezi


Klabu ya Arsenal imetangaza rasmi leo kuingia mkataba wa ushirikiano na Bodi ya Maendeleo Rwanda kwa msimu wa 2018/19.

Mkataba huo wa miaka mitatu unahusu nembo inayosomeka ‘Visit Rwanda’ (Tembelea Rwanda), ambapo itakaa kwenye upande wa kushoto katika jezi za Arsenal watakazovaa msimu ujao.

Kwa mkataba huo Rwanda, ndio watakuwa wadhamini pekee wa klabu ya Arsenal katika masuala ya utalii.

Uongozi wa Arsenal ulisema kwamba unawashukuru wadhamini hao ambapo nembo yao itaanza kuonekana kwenye jezi ambazo zitauzwa kwa ajili ya kutumika msimu ujao.

Rwanda ilitangaza kupita tovuti yake ikithibitisha kushirikiana na klabu ya Ligi Kuu England kama mdhamini rasmi katika sekta ya utalii.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba nyota mbalimbali ambao wamekuwa mashabiki wakubwa wa Wanyarandwa, pia watapata fursa ya kutembelea nchi hiyo iliyopo Afrika Mashariki.

Pia taarifa hiyo ya Rwanda iliongeza kuwa makocha wa klabu hiyo pia watapata fursa ya kukutana  na vijana wa nchi hiyo ili kuwajengea mbinu za maendeleo katika soka.

Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame ni miongoni mwa mashabiki wakubwa wa Arsenal na mara kwa mara amekuwa akionyesha mapenzi yake kwa klabu hiyo kupitia mitandao ya kijamii hasa Twitter.

Miongoni mwa mambo aliyoandika hivi karibuni ilikuwa ni tukio la kuondoka aliyekuwa kocha wa timu hiyo Arsene Wenger.

Rais huyo alimpongeza Wenger kwa kipindi chote alichoitumikia timu hiyo na kumtakia afya njema.