Arsene Wenger ajutia kukaa sana Arsenal

Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger

Muktasari:

Mrithi wa Wenger, Unai Emery tayari ameanza maandaizi ya msimu ujao wa Ligi

Paris, Ufaransa. Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema anadhani kosa kubwa zaidi alilopata kulifanya maishani mwake ni kukaa kwa miaka 22 ndani ya klabu hiyo ya London.

Wenger aliyejiuzulu kuinoa Arsenal mwishoni mwa Mei mwaka huu, aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na kituo cha Redio cha nchini Ufaransa cha RTL, akisema hilo ndilo kosa analolijutia zaidi.

Alisema ameyafahamu hayo baada ya kuondoka Arsenal aliyoinoa tangu mwaka 1996, akisema sasa amefahamu kwamba alitakiwa kuondoka mapema tofauti na alivyofanya.

“Nimebaini kuwa kosa kubwa zaidi nililowahi kulifanya maishani mwangu ni kukaa Arsenal kwa miaka 22, ingawa mimi napenda changamoto, lakini nadhani lilikua kosa kubwa sana kukaa pale kwa muda mrefu,” alisema Wenger.

Alisema kila mara wakati mashabiki wa klabu hiyo wakimnung’unikia aliona kama wanamuonea kwa kuamini alikua akiiongoza katika njia sahihi kumbe alikua anakosea.

Kocha huyo alisema kuwa hadi sasa bado hajajua atafanya nini baada ya kuachana na klabu hiyo, lakini anadhani baada ya kupumzika kwa miezi miwili au mitatu kuanzia sasa atafanya maamuzi ya hatima yake ya baadaye.

Ingawa Wenger alianza vema kazi yake klabuni hapo wakati ikiutumia uwanja wa Highbury, mambo yaliharibika kadiri siku zilivyosonga akishindwa kuipa mafanikio timu hiyo iliyohamia uwanja wa Emirates na kuzusha mvutano na kutoelewana baina yake na mashabiki.

Mrithi wa Wenger, Unai Emery tayari ameanza maandaizi ya msimu ujao wa Ligi lakini wengi wanataka kuona atasajili majina gani makubwa yatakayoweza kuwapa ubingwa.