VIDEO: Asasi za kiraia zatoa angalizo kwa Serikali ukusanyaji mapato

Meneja wa Uchambuzi Sera na Bajeti wa Policy Forum, Nicholas Lekule (katikati) akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, alipokuwa akitoa maoni ya kikundi kazi cha bajeti cha mtandao huo wa asasi za kiraia kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2018/2019. Walioambatana nae ni wanachama wa Policy Forum, Dominic Ndunguru (kushoto) na Rejoice Matanga. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Pia, asasi hiyo imewaomba wabunge kupitia mjadala wa bajeti wa siku saba unaoanza leo bungeni, kujikita katika kuikumbusha Serikali umuhimu wa kupanga bajeti inayotekelezeka.

Dodoma. Mtandao wa asasi za kiraia wa Policy Forum umesema endapo Serikali haitaweka mikakati dhabiti ya ukusanyaji wa mapato itakuwa ni ndoto kutekeleza bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/19.

Pia, asasi hiyo imewaomba wabunge kupitia mjadala wa bajeti wa siku saba unaoanza leo bungeni, kujikita katika kuikumbusha Serikali umuhimu wa kupanga bajeti inayotekelezeka.

Katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh32.5 trilioni, huku mapato ya ndani yakijumuisha ya halmashauri yakiwa ni Sh20.89 trilioni.

Katika mwaka wa fedha 2017/18, Serikali ilipanga kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya Sh19.99 trilioni ikijumuisha mapato yanayotokana na Serikali za mitaa. Hata hivyo, hadi kufikia Aprili makusanyo yalikuwa Sh14.83 trilioni ikiwa ni sawa na asilimia 75 ya makadirio.

Akiwasilisha maoni ya kikundi kazi cha bajeti cha mtandao huo jana, Meneja wa Uchambuzi Sera na Bajeti wa Policy Forum, Nicholas Lekule alisema pamoja na jitihada za Serikali za ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vya ndani, bado hayajakidhi mahitaji.

Alisema hali hiyo imesababisha miradi mingi ya maendeleo inayotegemea kutekelezwa kwa fedha za ndani kushindwa kutekelezwa.

“Kuna baadhi ya wizara hadi kufikia Aprili mwaka 2018 ama hazikuwa zimepokea kabisa fedha za maendeleo zilizopaswa kutoka kwenye vyanzo vyetu vya ndani au zilikuwa zimepokea fedha kidogo,” alisema.

Lekule alisema kutokana na sababu hizo, mtandao unawasihi wabunge kujikita katika mjadala mpana na wa kina katika namna bora zaidi ya kuboresha mapato.

“Ukusanyaji uwe wa haki unaoboresha uhusiano kati ya mlipa kodi na Serikali yake. Tungependa kuona walipa kodi wakiongezeka, huku mapato yakiongezeka pia,” alisema.

Alisema wanawasihi wabunge kujikita katika matumizi sahihi ya rasilimali na kuwapo nidhamu zaidi katika kinachopatikana kwa sababu taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zinaonyesha kuna fedha za Serikali zinazokusanywa hazitumiki ipasavyo.

Meneja huyo alisema ni vyema kuanisha sekta ambazo ukuaji wake ni muhimu zaidi katika uchangiaji wa ukuaji wa viwanda na kuzipa kipaumbele cha bajeti ili kufanikisha malengo yake.

Aliisihi Serikali kuendelea kuona umuhimu wa kuwekeza kimkakati ili kuleta tija zaidi katika utoaji wa huduma na kwamba, wangependa kuona sekta za kijamii kama vile elimu na afya zikiendelea kupewa kipaumbele kwenye bajeti.

“Serikali iangalie tatizo la upungufu wa watumishi kwenye sekta ya afya kwa kuhakikisha mikakati mizuri zaidi ya kuajiri na kuwabakisha katika ajira watumishi wa afya. Hii iambatane na kuboresha fursa za masomo kwa ajili ya kupata madaktari bingwa,” alisema.

Alishauri Serikali kuongeza bajeti kwenye sekta ya elimu na hasa ya maendeleo na iendane na kuifanyia kazi changamoto ya ucheleweshaji wa fedha katika maendeleo ya sekta hiyo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakulima Wanawake Wilaya ya Chamwino, Janeth Nyamayahasi aliiomba Serikali kuhakikisha pembejeo zinafika kwa wakati kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji nchini.

“Benki ya Kilimo ishuke hadi chini ili wakulima waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na benki hiyo. Ikiwezekana kwa sasa waweke wakala katika maeneo mbalimbali watakaosaidia katika kutoa mikopo kwa wakulima,” alisema.

Mwakilishi kutoka shirika la Sikika, Henry Sanuki alishauri Serikali kuweka jitihada katika kuongeza wataalamu wabobezi katika sekta ya afya kwa kusaidia kugharamikia mafunzo.

Alisema kwa kufanya hivyo kutawezesha hospitali za kisasa zilizojengwa na za mikoa kutoa huduma bora zaidi na kupunguza watu wanaosafiri nje ya nchi kutibiwa.