Ashangaa kuachwa aliyetaka kumhonga

Muktasari:

Ni katika kesi ya utoroshaji makontena 329 bila kulipiwa kodi

Shahidi wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi inayotokana na utoroshwaji makontena 329 katika Bandari Kavu ya Azam (AICD) bila kulipiwa kodi, amedai kuwa anasikitika kutomuona mahakamani mtu aliyetaka kumpa rushwa.

Shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo, Ashraf Khan, ambaye wakati wa utoroshaji makontena hayo ndiye alikuwa meneja mkuu wa AICD, alidai hayo wakati akihojiwa na wakili wa utetezi, Kung’e Wabeya.

Washtakiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Ufisadi, ni maofisa wa Azam ICD, maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ofisa wa kampuni ya uwakala wa mizigo ya Regional Service.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 110 yakiwamo ya kula njama kuidanganya Serikali, kuisababishia Serikali hasara ya Sh12.7 bilioni na utakatishaji fedha.

Wakati akitoa ushahidi wake wiki iliyopita huku akiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Timon Vitalis, shahidi huyo alidai baada ya kubaini utoroshwaji makontena hayo, alifika mtu ofisini kwake aliyemtaja kwa jina la Abdi akataka kumpa Sh10 milioni.

Mbali na hicho kiwango cha fedha ambacho kilikuwa kimefungwa kwenye mfuko wa karatasi, mtu huyo aliahidi kumuongezea kiwango kingine kama hicho ili kuzima uhalifu huo.

Hata hivyo, shahidi huyo alipokuwa akihojiwa na wakili Wabeya alipoulizwa iwapo hashangai mtu huyo aliyetaka kumpa rushwa hayupo mahakamani miongoni mwa washtakiwa, shahidi huyo kwanza alijibu kuwa hashangai, kisha akasema anasikitika kutomuona mahakamani.

Shahidi aliieleza mahakama kuwa rushwa nyingine ilikuwa Novemba 13, 2015 baada ya kubaini makontena manane hayaonekani na kwamba, baada ya kufanya mazungumzo (ofisini kwa aliyekuwa msimamizi mkuu wa kitengo cha ushuru wa forodha AICD, Eliachi Mrema (31), alirudi ofisini kwake na kumkuta huyo msomali Abdi akataka kumpa rushwa.

Alidai kuwa na fedha hizo zilizofungwa kwenye karatasi na yeye hakuzifungua maana alikuwa anaziogopa.