Ashikiliwa na polisi akituhumiwa kumbaka bibi wa miaka 85

Muktasari:

Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia  Daniel Colner (21) kwa tuhuma za  kumbaka bibi wa  miaka 85


Moshi. Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia  Daniel Colner (21) kwa tuhuma za  kumbaka bibi wa  miaka 85.

Mtuhumiwa anadaiwa kufanya kitendo hicho katika kata ya Kingachi wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Oktoba 17, 2018 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita amesema tukio hilo limetokea Oktoba 15, katika kata ya Kingachi wilayani Rombo.

Amesema Colner alivunja mlango wa nyumba ya bibi huyo na kumbaka.

Amebainisha kuwa baada ya kufanya kitendo hicho cha ubakaji, taarifa zilifika katika kituo cha polisi cha Wilaya ya Rombo na askari kuanza msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.

Ameseba bibi huyo alipofikishwa kituo cha polisi alibainika kuwa ameingiliwa kinguvu.

“Vipimo vya awali vinaonyesha kuwa bibi huyo alikuwa na manii na vipimo zaidi vinaendelea kufanyika. Polisi pia wamemkamata  kijana anayedaiwa kujihusisha na kitendo hicho huku uchunguzi ukiendelea,” amesema.

Hata hivyo mtuhumiwa huyo alipohojiwa na waandishi wa habari alikana kuhusika na tuhuma hizo huku akishangazwa na kitendo cha polisi kumkamata.

“Sihusiki na tuhuma hizi. Nilikuwa nyumbani ghafla nikashangaa  polisi  wamekuja na kunikamata kwa madai nimembaka bibi,” amesema Colner.