Ashtakiwa kwa kumiliki mali ya Sh1.4 bilioni

Muktasari:

  • Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter alimsomea Kimaro shtaka hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
  • Kimaro amefunguliwa kesi hiyo chini ya kifungu cha 27 (1)(4) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Meneja wa Fedha wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Prosper Kimaro amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kujilimbikizia mali zenye thamani ya Sh1.4 bilioni zisizolingana na kipato chake halali.

Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter alimsomea Kimaro shtaka hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Kimaro amefunguliwa kesi hiyo chini ya kifungu cha 27 (1)(4) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Anadaiwa kumiliki nyumba zenye thamani ya Sh1,178,370,334 na magari yenye thamani ya Sh307,364,678.20.

Wakili Peter alidai kuwa Kimaro amejilimbikizia mali zisizolingana na kipato chake kosa analodaiwa kulitenda kati ya mwaka 2012 na 2016.

Anadaiwa kuwa akiwa mtumishi wa umma wa TPA kama meneja wa fedha, katika eneo la Temeke alikutwa akimiliki mali zisizolingana na kipato chake halali cha zamani na cha sasa.

Mali hizo ni nyumba mbili zilizopo Mtaa wa Uwazi, Temeke zenye thamani ya Sh124.2 milioni na kiwanja kilichopo Yombo Vituka chenye thamani ya Sh12.9 milioni.

Zingine ni nyumba mbili zilizopo Temeke zenye thamani ya Sh63.5 milioni; na tatu zilizopo Temeke zenye thamani ya Sh159 milioni.

Kimaro anadaiwa kumiliki nyumba nyingine tatu zenye thamani ya Sh170.1 milioni; nyumba moja yenye thamani ya Sh71.3 milioni; kiwanja kilichopo Temeke chenye thamani ya Sh35 milioni.

Pia, kiwanja chenye thamani ya Sh25 milioni na amejenga nyumba tatu ambazo zina thamani ya Sh159 milioni; na nyumba nyingine yenye thamani ya Sh106 milioni.

Kadhalika, nyumba mbili zenye thamani ya Sh214 milioni; nyumba nne eneo la Viziwaziwa mjini Kibaha mkoani Pwani zenye thamani ya Sh199.7 milioni na moja iliyopo Kilimahewa, Tandika yenye thamani ya Sh70 milioni.

Kimaro anadaiwa kumiliki magari aina ya Toyota Land Cruiser lenye thamani ya Sh180.1 milioni na Mitsubishi lenye thamani ya Sh38.4 milioni. Anadaiwa pia kumiliki gari aina ya Toyota Harrier lenye thamani ya Sh35.8 milioni.

Pia anadaiwa kumiliki, Massey Ferguson yenye thamani ya Sh24 milioni na trela lenye thamani ya Sh4.5 milioni na Massey Ferguson nyingine yenye thamani ya Sh19.1 milioni na trela lenye thamani ya Sh4.8 milioni.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Kimaro aliyakana na Wakili Peter alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Wakili wa utetezi, Emmanuel Augustino aliiomba Mahakama kumpatia mteja wake dhamana; ombi ambalo halikupingwa na upande wa Jamhuri.

Hakimu Simba alitoa masharti ya dhamana akimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atatakiwa kuwasilisha mahakamani hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh200 milioni.

Mshtakiwa atatakiwa asitoke nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama na awasilishe hati zake za kusafiria mahakamani. Kimaro alishindwa kukamilisha masharti ya dhamana hivyo alipelekwa rumande.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 3 itakapotajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.