Asilimia 22 Mwanza ni maskini

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella

Muktasari:

Kwa mujibu wa tovuti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), mkoa huo una wanufaika 624,172 sawa na asilimia 22.5 ya wakazi wote wanaopaswa kupatiwa ruzuku.

Mwanza. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi 2012, Mkoa wa Mwanza ulikuwa na wakazi 2,772,509, kati yao 624,172 wanapaswa kupata ruzuku inayotolewa kwa kaya maskini.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), mkoa huo una wanufaika 624,172 sawa na asilimia 22.5 ya wakazi wote wanaopaswa kupatiwa ruzuku.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alizitaka kaya zinazonufaika na ruzuku hiyo  kuanzisha vyama vya akiba na mikopo (Saccos), huku akiwaagiza maofisa maendeleo ya jamii na  ushirika kuwatembelea wanufaika  ili kuwaelimisha namna ya kuanzisha Saccos maeneo yao.

Mongella alitoa kauli hiyo juzi alipowatembelea na kuzungumza na wanufaika wa mradi huo katika kata za Butimba na Mkuyuni, wilayani Nyamagana.

“Nitawachangia Sh1 milioni zitawekwa kwenye akiba ya kila mmoja wenu mtakapokamilisha taratibu za kuanzisha Saccos,” aliahidi Mongella.