Askari Magereza 11 wasimamishwa

Muktasari:

Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zinasema askari hao walisimamishwa kazi na Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa juzi.

Jeshi la Magereza Tanzania limewasimamisha kazi askari wake kumi na moja waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya mwanakijiji, Aloyce Makalla (41) wiki iliyopita.

Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zinasema askari hao walisimamishwa kazi na Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa juzi.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, John Masunga alithibitisha kusimamishwa kwa askari hao lakini hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi akisisitiza kuwa msemaji wa jeshi hilo ni Kamishna Jenerali pekee.

Askari waliosimamishwa ambao walishafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Korogwe mwishoni mwa wiki mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kassim Mkwawa ni Jonas Makere, Shadrack Lugendo, Lazaro Stephen, Mussa Zuberi, Ramadhan Yusuf, Robert Alfred, Fhidirish Osmas, Alfonce Revocatus, Mbesha Naftari, Hamis Msola na Michael Elias.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa hatua ya kuwasimamisha kazi askari hao imechukuliwa ikiwa ni kupisha vyombo vya sheria kufanya kazi yake kwa uhuru zaidi na kwamba hatima yao itategemea uamuzi wa mahakama hiyo.

Askari hao wa Wilaya ya Korogwe walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na shtaka la kumuua, Makalla, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kerenge wilayani humo.

Ilidaiwa mahakamani hapo na mwanasheria mwandamizi wa Serikali, Saraji Iboru kuwa Januari 22 saa 9.30 katika kitongoji cha Mapangoni Kijiji cha Kerenge, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua mwanakijiji huyo.

Iboru ambaye alikuwa akisaidiana na mwendesha mashtaka kiongozi, Shosa Naiman alidai kwamba siku ya tukio, washtakiwa hao walikwenda nyumbani kwa Makalla wakimtuhumu kwamba Januari 15 alimjeruhi askari mwenzao aitwaye Sajenti Stephen.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji. Hakimu Mkwawa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 15 itakapotajwa tena.