Askari wamtoa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai akiendesha kikao

Muktasari:

Hatua hiyo ilifanya baraza kukaa kimya kwa takribani dakika tatu kabla ya Mchovu kueleza kilichotokea juu ya askari hao kutaka asitishe shughuli za kuendesha kikao na kwenda nje kitendo ambacho alisema ni kinyume na taratibu za uendeshaji wa kikao cha baraza.

 Askari wawili wakiwa wamevalia kiraia wameingia kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichokuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu na kumpa kikaratasi chenye ujumbe wa kumtaka atoke nje ya kikao kwa ajili ya mazungumzo.

Hatua hiyo ilifanya baraza kukaa kimya kwa takribani dakika tatu kabla ya Mchovu kueleza kilichotokea juu ya askari hao kutaka asitishe shughuli za kuendesha kikao na kwenda nje kitendo ambacho alisema ni kinyume na taratibu za uendeshaji wa kikao cha baraza.

Alisema kabla ya kikao cha leo, Jumatatu, alipata taarifa ya kutakiwa kuripoti polisi na mkuu wa upelelezi wa wilaya bila kujua anachoitiwa na kutoa taarifa za kufika leo saa saba mchana baada ya kumaliza kikao cha baraza la madiwani.

"Nashangaa  tena kuona nikiletewa kikaratasi na askari wakati vikao vikiendelea... hili sio jambo la kawaida kwa kuwa wanakiuka taratibu. Wakati nikijiandaa kuingia kwenye kikao nilipokea simu kutoka nyumbani kwamba kuna askari saba wakiwa na silaha wamezunguka nyumbani wakinitafuta na sielewi kosa langu,” alisema Mchovu.