Monday, April 16, 2018

Askofu Mndolwa: Kanisa la Anglikana halijawahi kuwa na mpasuko

 

By Burhani Yakub, Mwananchi. byakub@mwananchi.co.tz

Askofu Mkuu Mteule wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Mahimbo Mndolwa anayetarajiwa kusimikwa rasmi Mei 20, mwaka huu katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Dodoma kushika wadhifa huo ameeleza mikakati yake.

Askofu Dk Mndolwa anajipanga kufanya mambo kadhaa katika miaka mitano ijayo ikiwamo kuhakikisha analisuka kanisa hilo ili liwe lenye kujitegemea zaidi ambapo mwaka 2020 atazindua rasmi mpango mkakati utakaotekelezwa na kanisa hilo.

Alitoa msimamo huo hivi karibuni wakati wa mazungumzo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa la Anglikana, mtaa wa Kilapula wilayani Muheza.

Swali: Kumekuwa na utata kuhusu historia yako hasa elimu ya dini, kuna tetesi kwamba ulisomea zaidi masuala ya kijeshi.

Inaendelea Uk 22

Inatoka Uk 21

Jibu: Historia yangu kifupi, nilizaliwa Novemba 24 mwaka 1969 pembezoni mwa Shamba la Chai la Ambangulu Kijiji cha Bagamoyo, Kata ya Vugiri wilayani Korogwe. Mwaka 1979 nikajiunga na Shule ya Msingi Bagamoyo na mwaka 1986 nikachaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Pugu hadi mwaka 1989 na mwaka 1990 hadi 1992 nikarudi Pugu kwa masomo ya kidato cha tano na sita nikichukua mchepuo wa sayansi (PCB) yaani fikizika, kemia na biolojia.

Mwaka 1993 nilikwenda Jeshi la kujenga Taifa Makutupora nilikoteuliwa kuendesha ndege za kivita, nadhani walioniona nikiendesha hizo ndege ndio wanaojiuliza nimekuwaje askofu.

Shahada ya kwanza ilikuwa niipatie Chuo cha Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Morogoro lakini sikumaliza baada ya Baba Askofu John Ramadhan kunichukua na kunipeleka Chuo cha Theolojia, ST Marks, Buguruni, Dar es Salaam na mwaka 1995 nikahamia Gremstom Afrika Kusini na Julai 1996 nikarudi ST Marks Buguruni lakini Novemba nilipokea barua ya kuteuliwa kuwa shemasi wa Kanisa la Mlalo Lushoto. Safari yangu ya utumishi wa Mungu iliendelea huku nikikatisha kwa kwenda masomoni katika vyuo vikuu vya nchi mbalimbali ikiwamo Ghana, Afrika Kusini na Marekani hadi Januari 1998 nilipoteuliwa kuwa kasisi nikahamishiwa Maramba wilayani Mkinga.

Januari 4, 2005 nilirudi ST Marks Buguruni kufundisha theolojia na mwaka 2009 nikateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shule ya Theolojia ya ST Marks. Nafasi ya Askofu Dayosisi ya Tanga niliipata nikiwa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu kilichopo Kwazulu Natal, Afrika Kusini nikichukua shahada ya uzamivu (PHD) na Septemba 4, 2011 nikasimikwa rasmi kuwa askofu wa Dayosisi ya Tanga hadi Februari mwaka huu nilipoteuliwa kuwa Askofu Mkuu Tanzania. Nina mke aitwaye Frida Madeni yeye ni muuguzi na tuna watoto wanne.

Swali: Ulijisikiaje ulipopata taarifa mara ya kwanza kwamba umeteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Tanzania?.

Jibu: Yalinitoka machozi ya uchungu, kwanza sikutegemea kama kuna siku ningeteuliwa katika wadhifa huu mkubwa, nilipokea uteuzi huu kwa mshangao mkubwa. Lakini pia nilipata uchungu hasa nikiziangalia changamoto zilizopo katika jimbo ninaloongoza la Tanga za uduni wa maisha ya waumini na jamii kwa ujumla, hilo ni jukumu zito mno kwangu. Unakutana na muumini wa kweli anatamani kuchangia kanisa lakini hana kitu ni masikini, inakupa uchungu unatokwa machozi kumhurumia, unalazimika kumsaidia tu.

Changamoto zilizopo katika jimbo langu la Tanga ni nyingi zinahitaji muda wangu mkubwa kuzitatua nililiwaza hili lakini nikakumbuka maandiko yanayosema “Mungu anaposema uwe huwezi kusema hapana, kwa hivyo nimepokea uteuzi na nitafanya kazi kwa unyenyekevu.

Swali: Ni vipaumbele gani ulivyojiwekea kutekeleza mara utakaposimikwa rasmi kuwa askofu mkuu?

Jibu: Kwanza nitakaa na maaskofu wa dayosisi zote na makasisi kuwasikiliza mawazo yao na nini kifanyike ili kusukuma mbele kanisa letu. Pili nitaendeleza mpango mkakati uliopo wa kanisa hadi ifikapo mwaka 2020 tutakapokuwa tukiadhimisha miaka 177 ya injili na miaka 50 ya Kanisa la Anglikana linalojitegemea Tanzania hapo tutazindua dira mpya. Unajua kitendo cha kupungua kwa kiasi kikubwa utegemezi wa ufadhili kutoka nje katika kanisa letu kumetusaidia kufikiri zaidi njia ya kutuvusha na tumefanikiwa.

Katika mpango mkakati utakaozinduliwa mwaka 2020 hadi 2025 utekelezaji

wake utaliwezesha kanisa kujitegemea zaidi kwani ujenzi wa makanisa utaongezeka, shule za kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu vikiwamo vya kitaaluma vitaongezeka na hata huduma za kijamii zitaongezeka.

Kupitia mpango huo mkakati kutakuwa na ongezeko la watumishi wa Mungu kwani uwezo wa kuwasomesha utakuwepo lakini kubwa zaidi ni kuwajengea uwezo waumini wa Anglikana na jamii kwa ujumla katika mambo ya ujasiriamali ili kuinua vipato vyao.

Hapo katikati tulirudi nyuma, Serikali ilitaifisha shule na vyuo vyetu, tunashukuru sasa ni ruksa kuanzisha hivyo ni jukumu letu kukazania hili na tutafanya.

Swali: Unashika wadhifa huu huku tukishuhudia mpasuko mkubwa ndani ya Kanisa la Anglikana, mpasuko uliosababisha watumishi wa Mungu kufarakana (mfano mgogoro uliowahi kulikumba kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam). Je una mikakati gani kuhakikisha inamalizika?

Jibu: Katika kanisa letu hakuna mpasuko bali ipo migogoro na kihistoria migogoro Anglikana ilikuwapo hata zamani kwa sababu ni sehemu ya jamii. Kwa mtazamo wangu, migogoro inapotokea, hutengeneza fursa ya kutafuta njia ya kukua kwa kanisa lakini pale inapoleta uchungu, maumivu na mateso kwa watumishi wa Mungu na hata waumini wenyewe, Mungu hili halitaki.

Kazi yangu kubwa itakuwa ni kwa kila aliyeumizwa namrejesha kwa upole ili amuabudu Mungu vyema. Niseme tu kwamba Mungu ana makusudio yake kunipa wadhifa huu, amenipa Uaskofu wa Tanzania ili anitume nimalize migogoro hii ambayo umeiita ni mpasuko, siamini kama ni mpasuko sababu kanisa halijapasuka.

Swali: Wanaokufahamu wanasema una misimamo hupendi ipindishwe, je katika kutumikia wadhifa huu wa kitaifa utalegeza misimamo?

Jibu: Nakubaliana na wewe, mimi ni kiongozi ninayetaka kufuatwa taratibu za kanisa, si misimamo yangu binafsi. Hapo kuna mambo manne, moja ni jambo lolote ambalo watu walizoea ukilirejesha katika taratibu lazima utatokea mtafaruku. Pili kuna shida kubwa ya uelewa wa mambo ya imani na taratibu zake katika hili nitalisimamia kikamilifu. Tatu kuna tatizo la kuacha maisha ya kikristona kufuata ya jadi, mila na tamaduni, nitoe tu mfano, waumini wetu wanaishi maisha duni, lakini wanapenda sherehe hujikuta wakiingia katika mikopo ili tu wanunue nguo mpya na kupika vyakula vya kifahari.hapa lazima tuwaambie, kipaimara si kuvaa au kula vizuri bali ni imani.

Sababu za kuyumba kwa imani moja wapo ni shule za kanisa kutaifishwa, mfano ni Tanga tulikuwa na shule zote zilitaifishwa lakini tunashukuru sasa Serikali imeruhusu tujenge tutajitahidi kwa sababu zinasaidia kuwapika waumini wakiwa na umri mdogo.

Swali…Tumeshuhudia Kanisa la Anglikana likiingia katika kashfa ya ushoga je nini msimamo wako?

Jibu: Dhambi ni dhambi, kazi yetu ni kuwaambia Kanisa la Marekani tubuni mrudi katika mstari wa kumtumikia Mungu. Katika hili, nitazungumza sana, nikienda Marekani nitawaambia uso kwa uso na wakija Tanzania nitawaambia bayana Kanisa Anglikana haliwezi kuvumilia kashfa hiyo.

Swali: Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) na Baraza la Maaskofu Katoliki wametoa matamko (waraka) kuhusu hali ya amani na kisiasa inavyoendelea nchini lakini Anglikana mpo kimya, unazungumziaje hili?

Jibu: Binafsi nafungwa kuzungumzia hili kwa sababu bado sijasimikwa kuwa askofu mkuu, ni swali ambalo angeulizwa kiongozi wangu Askofu Mkuu Dk Jacob Chimeledya. Maaskofu Anglikana tuna utaratibu wetu, pengine askofu mkuu akisema katika hilo la hali ya nchi na sisi tutapata nafasi ya kusema hicho ndicho au sicho.

-->