Askofu Shoo atuma salamu za rambirambi ajali ya kivuko

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo.

Muktasari:

  • Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo ametuma salamu za rambirambi kwa Rais John Magufuli

Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo ametuma salamu za rambirambi kwa Rais John Magufuli kutokana na ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere katika Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 170.

Kivuko hicho kilichokuwa kikitokea Bugolora wilayani Ukerewe kuelekea Kisiwa cha Ukara kilizama juzi mchana Septemba 20, 2018, ikielezwa kuwa kilikuwa na abiria zaidi ya 200.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za kanisa hilo mjini Moshi, Dk Shoo amesema msiba huo ni wa Taifa.

Dk Shoo amesema kufuatia ajali hiyo, kanisa hilo lipo pamoja na Watanzania katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

“Nitumie fursa hii kumpa pole Rais wetu kwa kuwa huu ni msiba wa kitaifa na tuko pamoja katika maombolezo haya,” amesema.

“Manusura wa ajali hii tuzidi kuwaombea Mungu awape uponyaji wa haraka. Poleni Watanzania wenzangu na Mungu azidi kuibariki nchi yetu.”

Title: Askofu Shoo atuma salamu za rambirambi ajali ya kivuko

Summary: Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo ametuma salamu za rambirambi kwa Rais John Magufuli