Askofu Shoo aunda tume mgogoro wa KKKT Mufindi

Muktasari:

  • Msimamo huo wa kanisa umetolewa na mkuu wa KKKT, Askofu Dk Fredrick Shoo, kufuatia tamko la waumini wa kanisa hilo Jimbo la Mufindi la kutaka waruhusiwe kuwa dayosisi kamili ya Mufindi.

Moshi. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limeunda tume maalumu kwa ajili ya kutafuta suluhisho la kudumu la mgogoro kati ya Jimbo la Mufindi na Dayosisi ya Kusini ya kanisa hilo.

Msimamo huo wa kanisa umetolewa na mkuu wa KKKT, Askofu Dk Fredrick Shoo, kufuatia tamko la waumini wa kanisa hilo Jimbo la Mufindi la kutaka waruhusiwe kuwa dayosisi kamili ya Mufindi.

Katika tamko hilo ambalo gazeti hili linayo nakala yake, waumini hao wanaokadiriwa kuwa 35,000 wamependekeza mipaka ya dayosisi hiyo iwe ni ile iliyokuwa ya Jimbo la Mufindi na maeneo jirani. “Mipaka ya dayosisi tarajiwa ya Mufindi ni ile iliyokuwa ya Jimbo la Mufindi na maeneo yatakayokuwa tayari kujiunga na Dayosisi ya Mufindi kufuata jiografia,” linasomeka tamko hilo.

“Vituo na taasisi zote zilizo ndani ya mipaka hiyo vitakuwa chini ya dayosisi tarajiwa. Mali zinazohamishika na zisizohamishika zitakuwa chini ya usimamizi wa wadhamini wa dayosisi”.

“Watumishi waliopo Jimbo la Mufindi watakuwa na hiari kubaki au kuhamia dayosisi nyingine na watumishi wa dayosisi nyingine yoyote watakaribishwa kujiunga na dayosisi tarajiwa ya Mufindi”

Katika tamko hilo, waumini hao wametaka watumishi waliopo ndani ya Jimbo la Mufindi wanaofanya kazi chini ya Dayosisi ya Kusini inayoongozwa na Askofu Isaya Mengele waondoke mara moja.

“Sisi wakristo wa Kilutheri Jimbo la Mufindi tunajiongoza na tutaendelea kujiongoza hadi taratibu zote za kusajili dayosisi mpya ya KKKT Mufindi zitakapokamilika chini ya ushauri wa KKKT,” wamedai.

Akizungumzia tamko hilo, Askofu Shoo alikiri kuwa walishalipokea na walilijadili, kisha wakaamua kuunda tume nyingine ya kanisa kushughulikia mgogoro huo.

“Nakiri tulilipokea hilo tamko na mara moja tulilijadili na kuunda tume nyingine ya Halmashauri Kuu ya kanisa kwenda kulishughulikia kwa kuzikutanisha pande mbili za mgogoro huo,” alisema.

Bila kutaja muundo wa tume hiyo na wajumbe wake, Askofu Shoo ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, aliwaomba waumini wa kanisa hilo kuwa watulivu wakati kanisa likisubiri matokeo ya tume hiyo.

Mgogoro huo unadaiwa kuibuka baada ya waumini hao kutumia haki yao kwa mujibu wa katiba ya KKKT, kuomba kuzaliwa kwa Dayosisi ya Mufindi, lakini uongozi wa Dayosisi ya Kusini ukagoma.

Kuanzia hapo, kumekuwa na matukio ya kutengwa kwa waumini wakidaiwa ni waasi na wengine kufunguliwa kesi polisi, vitendo ambavyo vimezidisha chuki na kuchochea zaidi mgogoro huo.