Askofu mwingine wa Anglikana ashtakiwa

Muktasari:

  • Dk Mokiwa ambaye alishtakiwa na kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali dhidi ya kanisa hilo, alivuliwa madaraka na Askofu Mkuu, Jacob Chimeledya.

Ikiwa imepita takriban miezi sita tangu aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa avuliwe madaraka na uongozi wa juu wa kanisa hilo, Baraza la Wazee wa Nyumba ya Walei wa Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), limeshtaki Askofu wao, Boniphace Kwangu.

Dk Mokiwa ambaye alishtakiwa na kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali dhidi ya kanisa hilo, alivuliwa madaraka na Askofu Mkuu, Jacob Chimeledya.

Katika mashtaka yake, baraza la walei la DVN limemuomba Askofu Chimeledya kutatua mgogoro baina ya waumini na askofu huyo uliodumu kwa miaka minne sasa.

Askofu Kwangu anatuhumiwa kwa mambo kadhaa ukiwamo ubadhirifu wa mali za kanisa.

Alipotafutwa kwa simu, askofu huyo alisema kwa kifupi kuwa, “Kuongea na mwandishi wa habari ni kupoteza muda wangu kama hayo yapo upo utaratibu.” Baada ya kauli hiyo alikata simu.

Akitoa tamko la wazee hao jana katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Nicholaus jijini Mwanza yalipo makao makuu ya dayosisi hiyo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Osoro Nyawanga alisema askofu huyo ameligawanya kanisa katika makundi.

Alisema hawajapata huduma za kiaskofu kwa kipindi cha miaka miwili, ikiwa ni pamoja na watoto kutopata kipaimara.

Nyawanga alisema licha ya viongozi wa kanisa hilo kulipigia kelele suala hilo kwa nyakati tofauti bado linazidi kushamiri.

Alisema Askofu Kwangu anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa mali za kanisa na kuwafukuza wachungaji huku akiwaweka anaowajua yeye na kwa miaka miwili sasa hajakalia kiti chake.

“Kuna fedha Sh190 milioni za International School iliyopo Isamilo jijini Mwanza, mali ya kanisa zimetafunwa na shule huenda itafungwa kwa sababu ina hali mbaya kwa sasa. Askofu hatumtaki tunapaza sauti askofu mkuu aje atumalizie mgogoro huu haraka, kanisa linaangamia na maendeleo yamekwama,” alisema Nyawanga

Waumini wazungumza

Muumini wa kanisa hilo, Peter Mlashani alisema mgogoro huo umekwamisha huduma nyingi za kanisa na kuwaathiri.

Joyce Abisai alisema, “Kweli kanisa linapoelekea ni pabaya hata nje ya kanisa tunakuwa na mwonekano na taswira mbaya.”