Ataka mazingira bora uwekezaji viwanda

Muktasari:

Ametoa ushauri huo kwenye kikao cha wadau wa kilimo  kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,  Amos Makalla kujadili fursa za uwekezaji wa viwanda na kilimo mkoani humo.

 

Mbeya. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT), Geoffrey Kirenga ameishauri Serikali kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa  mashirika na taasisi binafsi za kilimo au ufugaji ili kufikia uchumi wa viwanda.

Ametoa ushauri huo kwenye kikao cha wadau wa kilimo  kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kujadili fursa za uwekezaji wa viwanda na kilimo mkoani humo.

Kirenga amesema Serikali inapaswa kuimarisha uzalishaji wa mazao na kufanya kazi karibu na watu wanaojihusisha na kilimo.

“Hatuwezi kuzungumzia nchi ya viwanda kama Serikali haitaweka mazingira bora kwenye sekta ya kilimo. Angalia viwanda vyote vilivyopo hapa Mbeya malighafi zake zinategemea mazao ya kilimo na ufugaji, kama vile mahindi, shairi, ngano na maziwa,” amesema Kirenga.

Makalla amesema wamejipanga ili Mbeya ipige hatua za maendeleo katika biashara, utalii na  uwekezaji.