Tambwe Hiza kuzikwa kesho Dar

NDUGU JAMAA WASIMULIA SAA SITA KABLA YA KIFO CHA TAMBWE HIZA

Muktasari:

Mwanasiasa huyo aliyezaliwa mwaka 1959 alifariki ghafla juzi nyumbani kwake eneo la Mbagala Kizuiani wakati akijaribu kuwahi hospitali kwa tatizo la pumu ili kuokoa maisha yake.


Dar es Salaam. Kada maarufu wa Chadema, Richard Hiza Tambwe anatarajiwa kuzikwa kesho mchana katika makaburi ya Chang’ombe maduka mawili, Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo aliyezaliwa mwaka 1959 alifariki ghafla juzi nyumbani kwake eneo la Mbagala Kizuiani wakati akijaribu kuwahi hospitali kwa tatizo la pumu ili kuokoa maisha yake.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Februari 9, 2018 mdogo wa marehemu, Charles Hiza amesema kaka yake atazikwa katika makaburi hayo na hivi sasa wapo katika mchakato wa kupata eneo litakalotumika kwa ajili ya watu kutoa heshima zao za mwisho.

“Hapa nyumbani kwake ni padogo na hapatoshi kwa sababu watu watakuwa wengi,” amesema Hiza.

Tambwe Hiza katika harakati zake za kisiasa aliwahi kuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi, CUF na CCM kisha kuhamia Chadema mwaka 2015, mara ya mwisho kuonekana jukwaani Februari 7 eneo la Tandale kwa Tumbo akiwa miongoni mwa wana Chadema waliokuwa wakimnadi mgombea ubunge wa Kinondoni, Salum Mwalimu.