Atuhumiwa kutumia silaha kupora Sh40 milioni

Muktasari:

  • Kesi inayomkabili mkazi wa Kigamboni, Idd Hamad, anayetuhimiwa kutumia silaha kupora fedha na simu, imesikilizwa leo Mahakama ya Kinondoni

Dar es Salaam. Mkazi wa Kigamboni, Idd Hamad(25) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kujibu mashtaka mawili likiwamo la kutishia kutumia silaha kisha kupora Sh40 milioni.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi Isaya Kasako, leo Septemba 19,2018,  Wakili wa Serikali Nacy Mushumbuzi amedai katika shtaka la kwanza Mei 7, 2018 eneo la Mwananyamala alimwibia Said Haji fedha taslimu Sh600,000 na simu ya mkononi aina Sumsung yenye thamani ya Sh7.2 milioni baada ya kumtishia ili ampatie vitu hivyo.

"Mshtakiwa ulimwibia kwa kumtishia Haji huku ukijua ni kosa kwa mujibu wa sheria," alisema Mushambuzi.

Katika shtaka la pili katika tarehe hiyo hiyo eneo la Mwananyamala anadaiwa kuwa alimwibia Arafa Said Sh40 milioni baada ya kumtishia bastora na kisu ili ampatie vitu hivyo. 

Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa alikana makosa yote kutokana makosa hayo kutokuwa na dhamana. Hakimu Kasako aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 25,2018.