Auawa baada ya kukurupushwa akiiba

Muktasari:

  • Mtendaji wa Kata ya Butinya, Jacob Rafael alisema mtu huyo alikurupushwa wakati akiiba baada ya kuvunja duka la rejareja saa sita usiku wa kuamkia juzi.

Bukombe. Mtu mmoja ambaye hakutambulika, ameuawa kwa kupigwa kisha kuchomwa moto wa wananchi wa Kitongoji cha Isemabuna, Kijiji cha Butinzya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita akituhumiwa kuiba bidhaa zenye thamani ya Sh298,550 dukani.

Mtendaji wa Kata ya Butinya, Jacob Rafael alisema mtu huyo alikurupushwa wakati akiiba baada ya kuvunja duka la rejareja saa sita usiku wa kuamkia juzi.

“Baada ya kukurupushwa, mtuhumiwa aliyekuwa na usafiri wa pikipiki alitimua mbio, lakini wananchi waliwasiliana na wenzao na kufanikiwa kumkamata baada ya kuanguka akiwa njiani kuelekea eneo la Ushirombo,” alisema Rafael.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Isack Msengi alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo huku akiwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.