Aweso azindua miradi ya maji ya Sh546 milioni

Muktasari:

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amezindua miradi ya maji Temeke jijini Dar es Salaam na kuwataka wananchi waitumie vizuri ili iweze kudumu

 


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amezindua miradi ya majisafi Kibondemaji na uchakataji majitaka katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam inayogharimu Sh546 milioni.

Aweso amewataka wananchi wasikubaliane na watu wasioitakia mema Serikali kwa kuhujumu miundombinu hasa vishoka na watu wanaofanya maunganisho haramu ya maji.

Aweso ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 wakati akizindua miradi hiyo ambayo imetekelezwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) na Shirika la PDF chini ya Shirika la Water Aid Tanzania. 

“Miradi hii imetekelezwa kwa gharama kubwa hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kulipia huduma ya maji ili iweze kuendeshwa kwa ufanisi na iweze kufanyiwa marekebisho mara kwa mara, ili iwe endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo” amesema Aweso.

Akizungumzia miradi hiyo aliyoizindua, Aweso amesema mradi wa majisafi uliopo katika kata ya Kibondemaji na Charambe unalenga kuhakikisha upatikanaji maji safi na salama na kwamba utanufaisha wakazi wa Kibondemaji A, Kurasini mji mpya kata ya Charambe.

Amesema mradi huo, una urefu wa Kilomita 11 na kisima chenye urefu wa mita 180 chenye uwezo wa kutoa maji kiasi cha lita 224,000 kwa siku, ikijumuisha vibanda saba vya kuchotea maji na kwamba gharama za mradi huu ni Sh 187 Milioni.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva ametangaza kiama kwa watu wote watakaojihusisha na wizi wa maji.

Lyaniva amesema wilaya ya Temeke ina kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji na katika kata 23,  kata  10 zinapata maji ya Dawasa ila 13 hazipati. Hivyo wana uhitaji mkubwa wa maji hasa katika maeneo ya pembezoni.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja amesema amepokea maelezo na kwamba wanatakiwa ifikapo mwaka 2020, wawe wamefikisha asilimia 95 ya maji kwa Jamii.

Amesema maji yanatakiwa kumfikia mwananchi aliyeomba kupatiwa maji ndani ya siku saba na atakayecheleweshewa atoe taarifa.