Azam kuongeza ushindani soko la mawasiliano

Muktasari:

Kwa sasa kuna watumiaji zaidi ya milioni 40 wa simu za mkononi waliosajiliwa

 Watumiaji wa huduma za simu nchini watakuwa na machaguo mengi zaidi baada ya kampuni ya Azam kupewa leseni ya kuanza kutoa huduma hizo.

Kampuni mpya ya Azam Telecommunications Limited inaongezeka sokoni ili kuongeza ushindani kwenye mauzo ya data za intaneti, muda wa maongezi na huduma nyingine baada ya kupewa masafa ya 2 x 10 MHz kwenye mnada ulioigharimu Dola 10 milioni za Marekani (zaidi ya Sh22.5 bilioni).

Taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), iliyotolewa hivi karibuni inasema mnada uliofanyika Juni 8 Azam na Vodacom ziliibuka washindi.

“TCRA inapenda kuwatangaza washindi wa masafa ya 2 x 20 MHz yaliyopo kwenye spectrum ya 700 MHz. Vodacom imepata masafa ya 2 x 10 MHz na kulipa jumla ya Dola 10.005 milioni za Marekani (zaidi ya Sh22.511 bilioni) na kufanya jumla ya mapato ya mnada huo kuwa Dola 20.005 milioni (zaidi ya Sh45.011 bilioni),” inasomeka sehemu ya taarifa ya TCRA. Mnada huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ya mwaka 2016 inayolenga kukuza uwekezaji na ubunifu wa kisayansi.

Pia, sera hiyo inakusudia kuongeza idadi ya watumiaji huduma za intaneti wafike asilimia 60 mwaka 2021 na asilimia 90 mwaka 2024.

“TCRA inawapongeza Azam Telecommunications na Vodacom kwa kufanikiwa kupata masafa hayo. ni matarajio yetu kutakuwa na tija kijamii na kiuchumi hasa kwenye huduma za afya, elimu, kilimo, fedha, biashara na Tehama,” imesema TCRA.

Kwa sasa, kuna watumiaji milioni 19.3 wa intaneti ambayo usambaaji wake mwaka jana ulikuwa asilimia 45.

Msemaji mkuu wa kampuni ya Azam, Hussein Sufian alisema muda wowote kuanzia sasa utaratibu mwingine utakapokamilika, Watanzania wataanza kufurahia huduma za kampuni hiyo ambazo zitakuwa na bei ya chini zaidi.

Naye ofisa operesheni mkuu wa Vodacom, Diego Gutierrez alisema masafa hayo yatasaidia kuimarisha huduma kwa wateja wake nchini.

“Yatatusaidia kutekeleza mipango yetu ya kuongeza usambaaji na ubora wa huduma hasa watumiaji wa mtandao wa 4G,” alisema.