Azam yatoa ufafanuzi mitandao yao kutoonekana hewani

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Azam Media Limited (AML), Tido Mhando ametoa ufafanuzi wa kutoonekana hewani kwa mitandao yao ya kijamii.

Akizungumza na MCL Digital, Tido amesema walifuata maelekezo ya TCRA iliyowataka watoa huduma wa mitandao ya kijamii ambayo bado haina leseni kutoendelea na huduma hiyo.

“Tumekamilisha masuala yote ya usajili, tumelipa kila kitu, tunachosubiri ni kupewa tu leseni, tutarudi hewani muda wowote,” amesema Tido.

“Si kweli kwamba tumefungiwa au kusimamishwa, ni sisi wenyewe tuliacha kutoa huduma ili kufuata maelekezo ya TCRA, lakini tutarudi kwa sababu tumemaliza kila kitu.”