VIDEO: Baada ya kutoka jela Dodoma afuata redio ya bendi mbili Mwanza

ALIYEPEWA MSAMAHA WA RAIS ARUDI MWANZA KUCHUKUA REDIO YAKE YA MKULIMA

Muktasari:

George Kayanda (78), mzaliwa wa Kijiji cha Igagala wilayani Kaliua mkoani Tabora, alikuwa akitumikia kifungo cha maisha jela.

 Mfungwa katika Gereza la Isanga mkoani Dodoma aliyenufaika na msamaha uliotolewa na Rais John Magufuli badala ya kurejea kwao, ametua jijini Mwanza kufuatilia redio yake ya bendi mbili aliyoiacha siku alipokamatwa.

George Kayanda (78), mzaliwa wa Kijiji cha Igagala wilayani Kaliua mkoani Tabora, alikuwa akitumikia kifungo cha maisha jela.

Kayanda alihukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa mwaka 1990 baada ya kukaa mahabusu tangu mwaka 1980 shauri lilipokuwa likisikilizwa.

Alibadilishiwa adhabu kuwa kifungo cha maisha mwaka 2006 kabla ya Desemba 9, Rais Magufuli kutoa msamaha kwa wafungwa 8,157 yeye akiwamo wakati wa maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika.

“Siku nakamatwa kwa kosa la mauaji ya mtu aliyenivamia eneo langu la kazi nikiwa mlinzi, niliacha redio yangu ya bendi mbili ambayo ni kati ya vitu vyangu vya thamani nilivyokuwa nikimiliki,” alisema Kayanda akizungumza na Mwananchi jana eneo la stendi kuu ya mabasi ya Nyegezi jijini Mwanza.

Alisema ameshamwelekeza ndugu yake alikofikia huko Bwiru alikokuwa akifanya kazi ili kufuatilia redio hiyo. “Kwa ajili ya usalama wangu siwezi kufika pale nilipokuwa nikilinda, naweza kukutana na ndugu wa marehemu yakawa mengine makubwa zaidi,” alisema.

Kayanda alisema, “Kikubwa nataka redio yangu. Nikishaipata ndipo nitaanza kutafuta namna ya kwenda nyumbani kwangu Kaliua, naambiwa imekuwa wilaya siku hizi.”

Hata hivyo, alisema hana uhakika wa uhai na walipo mkewe Fillister Kayanda na watoto wake watano; Pizomu Ndabire, Ramesi Kayanda, Dorothea Roy, Foadi Furaha na Yoram Kayanda kutokana na kupoteza mawasiliano nao tangu alipofungwa.

Kilichosababisha afungwe

Akizungumza kwa uchangamfu, Kayanda alisema kilichosababisha ashtakiwe na kuhukumiwa adhabu ya kifo kabla ya kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha ni tukio la mwaka 1980.

Alisema alipambana na kumuua mmoja kati ya watu wawili waliomvamia akiwa lindo kwa nia ya kuiba mali za mwajiri wake ambaye hamkumbuki jina.

“Wale watu walifika wakijidai kugombana wao kwa wao, lakini ghafla wakanivamia. Nilipambana nao na kumuua mmoja; mwingine alikimbia,” anasimulia.

Alisema ingawa alijitetea kujiokoa na kukoa mali ya mwajiri, kibao kilimgeukia na kujikuta akikamatwa, kushtakiwa na hatimaye kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa mwaka 1990, baada ya kukaa mahabusu katika Gereza la Butimba kwa miaka 10.

Akiwa jela alisema alitegemea sala, “Imani katika dini na kusali rozari kila siku kwa miaka yote 37 niliyokaa gerezani ilinifanya niwe na imani kuwa ingawa kifungo changu ni cha maisha ipo siku Mungu atatenda muujiza wa kunitoa gerezani.”

Alisema Desemba 9 itasalia katika kumbukumbu yake baada ya kusikia jina lake likitajwa likiwa namba nne kwenye orodha ya wafungwa 15 waliosamehewa kutoka Gereza la Isanga.

“Sala yangu ya rozari kila siku imejibu kwa Rais Magufuli kukohoa tu, na amri yake ya kututoa gerezani kutekelezwa mara moja,” alisema Kayanda aliyetoka jela Desemba 10, siku moja baada ya msamaha huo.

Kuhusu maisha ya jela alisema, “Ni ya shida na tabu. Ni heri kuonekana mjinga, mwoga na dhaifu unapochokozwa kuliko kupigana na kujikuta ukiishia gerezani.”

Alisema maisha ya jela yalimfanya kumrejea Mungu na alipewa jina la nabii na wafungwa wenzake kutokana na tabia na ratiba yake ya maombi akisema ataendelea nayo.