Baba atuhumiwa kumfanya bintiye wa miaka 5 mkewe

Muktasari:

  • Majirani wadai mtoto amekuwa akilia usiku mara kwa mara anapoulizwa mtuhumiwa hudai washirikina ndiyo humsumbua

Geita. Katika hali isiyo ya kawaida, mwanaume aliyetambulika kwa jina la Melon Joseph (25) mkazi wa Nyarugusu wilayani Geita, anadaiwa kuishi kinyumba na mtoto wake wa miaka mitano na kumgeuza kuwa mkewe.

Kutokana na tuhuma hizo, mtuhumiwa huyo anashikilia kwa uchunguzi huku kamanda wa polisi mkoani hapa, Mponjoli Mwabulambo akithibitisha tukio hilo.

Mponjoli alisema uchunguzi wa awali inadaiwa mtoto huyo ameingiliwa kimwili na kwamba tukio hilo liligundulika Septemba 18, wakati jirani akimuogesha mtoto huyo alibaini kuwa anasikia maumivu sehemu zake za siri.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi na ikibainika kwamba kweli mtoto huyo ameingiliwa na mtuhumiwa, sheria itachukua mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Mary Juma mkazi wa Buziba Kata ya Nyarugusu alidai kumbaini mtoto huyo kufanyiwa ukatili baada ya kumuita ili amuogeshe lakini alikataa kupanua miguu ili amsafishe.

“Nilikuwa nawaogesha wanangu na yeye alikuwa anacheza nao nikaona kwa kuwa ni mchafu nimuoshe na yeye maana mama yake hayupo na baba hashindi nyumbani, lakini nilipokuwa namuosha alikuwa hataki kusogeza mguu nikamuuliza akakataa kusema.

“Nikashtuka maana alianza kutokwa na machozi nikaingia naye ndani nikamwambia aniambie shida yake nitamnunulia soda, ndiyo akaniambi baba yake humuingilia kila siku usiku niliwaita wanawake wengine majirani zangu nikawaeleza tukaamua kwenda kuripoti,” alisema Mary.

Majirani hao walisema mtuhumiwa huyo ambaye ni fundi baiskeli mtaani hapo, aliachana na mkewe muda mrefu na kubaki na mwanaye.

Mtoto huyo, alidai baba yake humuingilia mara kwa mara usiku na amekuwa akilia kwa sauti lakini hakuna wa kumsadia huku baba yake akimtisha akisema atampiga.

“Naumia kila anaponiingia nalia, lakini aliniambia nisimwambie mtu nikiulizwa kwa nini nalia usiku niseme natokewa na washirikina … nataka nirudi kwa mama sitaki tena kukaa na baba,” alisema.

Zaitun Ally ambaye ni jirani, alisema mtoto huyo amekuwa akilia usiku na wanapohoji asubuhi mtuhumiwa hudai mwanaye anaandamwa na washirikina ambao wamekuwa wakimsumbua na kumfanya aweweseke.

“Alipokuja na mtoto hapa tulimhoji alipo mama yake akadai wameachana, tukamshauri ampeleke kwa bibi yake akakataa akidai bibi anamcheza (anamroga) mwanaye, tukamwambia hana hata dada atakayekubali kukaa naye akadai watamtesa kumbe yeye ndiye shetani,” alidai Zaitun.

Alisema hata nyumba aliyokuwa akiishi kabla ya kuhamia kwenye eneo hilo, mtoto huyo inadaiwa alikuwa akilia sana na alipokuwa akiulizwa na majirani, mtuhumiwa aliwajibu kuwa ni washirikina humfuata mwanaye na kumfanya aweweseke.