Baba mbaroni akidaiwa kukeketa mabinti zake

Muktasari:

  • Awali, watoto hao wenye umri chini ya miaka 18, waligoma kukeketwa

Arusha. Mkazi wa Kijiji cha Oloipili wilayani hapa mkoani Arusha anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwapeleka kwa nguvu mabinti zake wawili kukeketwa.

Akizungumza jana katika maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo Serikali imepanga kuadhimisha leo badala ya Juni 16, Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani Ngorongoro, kitengo cha dawati la jinsi, Lilian Ngunito alidai kuwa mzazi huyo ambaye ni mmoja wa viongozi wa Serikali kijiji cha Oloipili alilazimisha kukeketwa watoto hao baada ya kuwapeleka kwa ngariba.

“Ni kweli tulipata taarifa za kulazimisha watoto wake kukeketwa na taarifa tukazifikisha polisi ambao tayari wamemkamata hadi jana alikuwa rumande,” alisema.

Mama mdogo wa watoto hao, Nina Ole Minisi alisema kiongozi huyo aliwapeleka watoto hao kukeketwa siku chache baada ya mama yao kufariki dunia.

“Hawa watoto ni wadogo, baada ya mama yao kufariki dunia, ndipo baba yao alianza mikakati kwa kushirikiana na mangariba kuwakeketa na walifanikiwa juzi Jumapili,” alisema.

Alisema awali, watoto hao wenye umri chini ya miaka 18, waligoma kukeketwa lakini, baba yao aliwalazimisha na kutishia kujiua kama wasipokubali kukeketwa.

“Nilizungumza nao kabla ya tukio hilo na waliomba msaada tuwasaidie wasikeketwe lakini kutokana na shinikizo la baba yao na kutishia kujiua ndipo walikubali kwa shingo upande,”alisema.

Hata hivyo, alisema baada ya kukeketwa walizuiwa kusema hadi juzi, ilipobainika kupelekwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Ngorongoro ya Wasso na kuwakuta tayari wamekeketwa na wamepata madhara.

“Ilibidi walazwe hospitali ili kupata matibabu kwani walikuwa wameharibiwa sana na jana (juzi) ndio wameruhusiwa kutoka hospitali.

“Kuna mpango wa kumwachia (mtuhumiwa) sisi kama familia hatujui hatima ya watoto hawa. Mimi niliomba kuwachukua baada ya mama yao kufariki dunia lakini baba yao aligoma,” alisema Minisi.

Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii, mkoa wa Arusha, Saimon Panga alisema ofisi yake inafuatilia kwa karibu tukio la kiongozi huyo kukeketa watoto na tayari hatua za kisheria zimeanza.