Babu Seya, Papii Kocha waanza kuingia studio

BABU SEYA, PAPII WAANZA MAKEKE

Muktasari:

Baada ya msamaha huo, familia ya wanamuziki hao ilikwenda Ikulu kumshukuru Rais Magufuli

Dar es Salaam. Wanamuziki Nguza Vicking maarufu ‘Babu Seya’ na mwanae Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ wameanza maandalizi ya ujio wao mpya katika muziki, ikiwa ni zaidi ya miaka 14 tangu walipoachia nyimbo zao mpya.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Januari 22, 2018 imesema wawili hao wameanza na upigaji wa picha,  jambo walilokiri kuwa geni kwao kutokana na mazingira ya ufanyaji muziki hivi sasa kuwa tofauti na ya zamani.

Babu Seya, ambaye ni mtunzi wa kibao maarufu cha “Seya”, na mwanaye Papii Kocha wameshirikiana katika wimbo huo, ni miongoni mwa wafungwa 8,157 waliosamehewa na Rais John Magufuli siku ya Uhuru wa Tanganyika.

Walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa na adhabu za vifungo vya maisha na kunyongwa ambayo si rahisi kupata msamaha wa kawaida wa mkuu wa nchi unaotoleewa siku ya sherehe hizo.

 

Baada ya msamaha huo, familia ya wanamuziki hao ilikwenda Ikulu kumshukuru Rais Magufuli na siku chache baadaye Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza aliwakutanisha na uongozi wa studio ya Wanene iliyokubali kuchukua jukumu la kuwarejesha tena katika muziki.

 

Taarifa hiyo imesema wanamuziki hao tayari wameanza kuandaa kazi mpya katika studio hizo kubwa na bora zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

 

“Wameanza kwa kufanya photoshoot (upigaji picha) kitu ambacho wamekiri kuwa ni kigeni mno kwao kutokana na kuwa gerezani kwa miaka 14 na wametoka katika nyakati ambazo muziki wa Tanzania umepiga hatua kubwa ukilinganisha na zamani,” imesema taarifa hiyo.

Akizungumzia ujui wao mpya Papii Kocha amesema, “Miaka 14 si mchezo, mambo kama haya si unayaona mwenyewe niliyakosa. Nimemiss vitu vingi kama picha za ukweli, mambo haya kule tulipotoka hamna. Lazima uelewe hii ni dunia nyingine.”

Papii Kocha amesema nyimbo zao mpya zitakuwa nzuri zaidi kuliko za zamani, “Hiyo ni kwa sababu tumejipanga vizuri na kazi zinazokuja zitakuwa nzuri zaidi ya zile tulizofanya mwanzo.”