Babu Seya, Papii Kocha waula tena

BABU SEYA NA WANAWE WATINGA IKULU, WATETA NA RAIS MAGUFULI

Muktasari:

Wawili hao na wanafamilia wengine wawili, jana walipata nafasi ya nadra kuingia Ikulu na kuzungumza na Rais John Magufuli, ikiwa ni siku 25 tangu waliposamehewa kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi na kubaka watoto wenye umri kati ya miaka sita na nane.

Dar es Salaam. Unaweza kusema wanamuziki maarufu wa muziki wa dansi, Nguza Mbangu Vicking, maarufu kwa jina la “Babu Seya” na mwanaye, Johnson Nguza au “Papii Kocha” wamepata bahati nyingine ya kipekee.

Wawili hao na wanafamilia wengine wawili, jana walipata nafasi ya nadra kuingia Ikulu na kuzungumza na Rais John Magufuli, ikiwa ni siku 25 tangu waliposamehewa kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi na kubaka watoto wenye umri kati ya miaka sita na nane.

Babu Seya, ambaye ni mtunzi wa kibao maarufu cha “Seya”, na mwanae Papii Kocha ambaye wameshirikiana katika wimbo huo, ni miongoni mwa wafungwa 8,157 waliosamehewa na Rais Magufuli siku ya Uhuru wa Tanganyika.

Walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa na adhabu za vifungo vya maisha na kunyongwa ambazo si rahisi kupata msamaha wa kawaida wa mkuu wa nchi unaotolewa siku ya sherehe hizo.

Mbali na kusamehewa, Nguza alitajwa jina na Rais Magufuli katika hotuba hiyo pamoja na mfungwa mwingine anayejulikana kwa jina la Matonya, kitu ambacho si cha kawaida kutajwa jina miongoni mwa wafungwa zaidi ya 8,000.

“Najua mmekuwa mkihangaika kutaka kuniona nikaona wacha niwasikilize,” anasema Rais katika taarifa ya Idara ya Mawasiliano ya Rais iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana.

“Hata hivyo, mshukuruni Mungu ambaye ndiye hutoa msamaha. Sasa nendeni mkachape kazi na mumtangulize Mungu.”

Wawili hao walihukumiwa mwaka 2004 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na juhudi zao kukata rufaa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ziligonga mwamba na hivyo kulazimika kusubiri “neema za Mungu”.

Baada ya kutoka katika Gereza la Ukonga Desemba 9 saa 12:00 jioni na kupokewa na mashabiki na ndugu zao, wawili hao waliahidi kwenda kumshukuru Rais Magufuli, lengo ambalo jana walilitimiza wakiwa pamoja na wanafamilia wengine Nguza Mbangu na Francis Nguza.

“Yaani sijui nisemaje? Hapa nina furaha kubwa sana moyoni mwangu,” Nguza anasema katika taarifa hiyo ya Ikulu.

“Nilikuwa naomba sana tangu muda mrefu nikutane naye. Nimeomba sana sana, hatimaye leo nimefanikiwa na nimemwambia namshukuru sana kwa kutusamehe na sasa nipo tayari kuchapa kazi,” alisema Nguza.

Picha zilizotumwa na idara hiyo zinamuonyesha Nguza na watoto wake, Papii Kocha, Nguza Mbangu na Francis Nguza wakiwa katika picha ya pamoja na Rais na nyingine zikiwaonyesha wakisalimiana na baadaye kutoka Ikulu.

Babu Seya na Papii Kocha waliishi katika Gereza la Ukonga kwa miaka 13 na miezi minne wakikabiliwa na kosa la kubaka na kulawiti watoto 10 wa kike ambao walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza Dar es Salaam.

Kupitia taarifa ya Ikulu iliyosainiwa na Gerson Msigwa, mkurugenzi wa idara hiyo ya mawasiliano, Nguza na familia yake walimuombea Rais huku msemaji wa familia hiyo, Nguza Mbangu akibainisha kuwa wanamuziki hao sasa wataendelea na kazi yao ya sanaa.

Baada ya kuzungumza na Rais, Papii Kocha alisema: “Ameturuhusu kufanya kazi na watu wategemee kuwa muda si mrefu watapata vitu vizuri. Tumekuja kuukomboa muziki wa dansi maana naona kama kuna vitu vilikuwa havijakaa sawa.”