Babu Tale afunguka kupigwa marufuku wimbo wa Mwanza

Muktasari:

  • Meneja wa lebo ya Wasafi, Babu Tale amesema wamepokea maagizo ya Baraza la Sanaa (Basata) kuhusu kufungiwa kwa wimbo wa ‘Mwanza’ na kuahidi kuufanyia kazi kwani ndiyo mzazi wao.

Dar es Salaam. Baada ya Baraza la  Sanaa la Taifa (Basata) kuupiga marufuku wimbo wa ‘Mwanza’ ulioimbwa na wasanii Diamond na Rayvanny na kutaka usichezwe wala kuonyeshwa mahala popote pale, Meneja wa lebo ya Wasafi, Hamis Taletale’Babu Tale’ amefunguka.

Akizungumza na Mwananchi leo Babu Tale amesema wameyasikia maagizo yote yaliyotolewa na baraza hilo na kuahidi kuyafanyia kazi.

Amesema pamoja na kwamba hawaoni tatizo lililopo katika wimbo huo kwa kuwa lugha zilizotumiwa ni za kisanii lakini hawana budi kutekeleza maagizo ya Basata kwani ndio mzazi na mlezi wao.

Alipoulizwa ni kwa nini hawakupeleka nyimbo zao kuhaririwa Basata kabla sheria inavyosema kabla ya kuziachia kwa jamii, meneja huyo amesema wamejifunza kupitia hilo na kuanzia sasa watakuwa wakifanya hivyo.

Kuhusu wasanii wao kutakiwa kuufuta, Babu Tale amesema watahakikisha wanafanya hivyo japokuwa mpaka kufika saa 11:09 wimbo huo ulionekana bado upo katika ukurasa wa akaunti ya Diamond.

Hata hivyo, alipotakiwa kueleza kuwa haoni kama mwendelezo wa kuendelea kufungiwa nyimbo za wasanii kutoka lebo hiyo  inawashushia heshima yao kwenye jamii.

 “Sidhani kama hilo lina tatizo na ndio maana kila siku wasanii wetu wanatoa nyimbo mpya na zinazopokelewa vizuri sokoni, labda tatizo ni lugha ya sanaa ambayo imekuwa ikitumika baadhi ya watu hawaielewi,” amesema

“Pia ieleweke nyimbo zote zinazotoka Wasafi hazipitiwi na mtu mmoja kabla hazijachiwa, kila mtu ana mchango wa kuangalia wapi pamekaa ndivyo sivyo na kurekebisha,” ameongeza

Leo Katibu wa Basata, Godfrey Mngereza ametangaza kuupiga marufuku wimbo wa Mwanza ambao pamoja kuwa na siku ya pili tangu kuachiwa umeshika nafasi ya kwanza ya wimbo uliotazamwa kwenye mtandao wa Youtube kwa kuwa na watazamaji zaidi ya milioni moja.