Babu Tale asubiri hatima yake mahakamani

Mmoja wa Mameneja wa Diamond,BabuTale (mwenye trakisuti ya kijivu) akisindikizwa na askari polisi kuingia Mahakama kuu Mei 23, akikabiliwa na kesi ya madai dhidi ya Sheikh Hashim Mbonde.Tale ameshindwa kumlipa sheikh huyo Sh 260 milioni na Mahakama Kuu kutoa amri akamatwe.PICHA|OMAR FUNGO

Muktasari:

Analazimika kukaa mahabusu kwa muda usiojulikana

Dar es Salaam.  Mkurugenzi wa Kampuni ya Tiptop Connection, Hamis Shaban Taletale maarufu Babu Tale anaendelea kusubiri  hatima yake baada ya leo Mei 24, 2018 kufikishwa tena katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

 Jana, Mahakama hiyo ilimuamuru Babu Tale kukaa mahabusu katika kituo cha Polisi akisubiri amri ya kupelekwa kifungoni katika Gereza la Ukonga.

 Mahakama hiyo ilitoa uamuzi uliotolewa na Naibu Msajili, Wilbard Mashauri Februari 16, 2018, iliamuru Babu Tale na ndugu yake Idd Shaban Taletale wakamatwe na kupelekwa kifungoni katika gereza la Segerea baada ya kushindwa kutekeleza hukumu yake.

 Katika hukumu hiyo iliyotolewa na  Jaji Agustine Shangwa Februari 18, 2016 iliwaamuru ndugu hao kumlipa fidia ya Sh250milioni, Mhadhiri wa Dini ya Kiislam Sheikh Hashim Mbonde, kutokana na makosa ya kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake.

 Kutokana na amri hiyo ya kukamatwa, Babu Tale alitiwa mbaroni juzi na kupelekwa mahakamani hapo kwa ajili ya amri ya kumpeleka kifungoni, lakini alilazimika kurudishwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi kwa kuwa Naibu Msajili aliyetoa amri ya kuwakamata hakuwapo, kurudishwa mahabusu mpaka atakaporejea.

 Kwa kuwa haijulikani ni lini atarejea, Babu Tale atalazimika kukaa mahabusu kwa muda usiojulikana mpaka Naibu Msajili Mashauri atakaporejea.

 Leo, amefikishwa mahakamani hapo na hadi leo alasiri haijajulikana kama ameletwa kulipa fidia ya Sh250milioni anayodaiwa, kupewa dhamana au kupelekwa gerezani kuanza kutumia kifungo.