Bajeti Wizara ya Mambo ya Nje yapitishwa

Muktasari:

Uamuzi wa kupitishwa bajeti hiyo na Bunge kuahirishwa uliwagawanya wabunge

 


Dodoma.  Kitendo cha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje mwaka 2018/19 kupitishwa leo mchana Mei 23, 2018 na kikao cha Bunge kuahirishwa hadi kesho, kimewagawa wabunge.

Bajeti ya wizara hiyo ya ShSh177bilioni iliyowasilishwa bungeni leo asubuhi na Balozi Augustine Mahiga na kujadiliwa na wabunge wasiozidi 10, haikupata upinzani kutoka kwa wabunge kama zilivyo bajeti nyingine tangu kuanza kwa Bunge la bajeti Aprili 3, 2018. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ameahirisha kikao hicho saa 7:45 mchana.

Ilipofika saa 6:45 mchana, dakika 15 kabla ya muda wa kawaida wa kuahirisha kikao cha Bunge hadi saa 10 jioni, Dk Tulia aliongeza nusu saa ili kutoa fursa kwa Balozi Mahiga na Naibu wake, Dk Susan Kolimba kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge.

Baada ya mawaziri hao kujibu, Bunge lilikaa kama kamati  kupitisha bajeti hiyo, baadaye Dk Tulia aliongeza tena nusu saa ambapo hakukuwa na mbunge aliyehoji jambo lolote wakati wa kupitisha vifungu hivyo.

Ilipofika saa 7:45 mchana, kikao hicho kiliahirishwa hadi kesho saa 3 asubuhi ambapo wabunge mbalimbali waliozungumza na MCL Digital, wamekuwa na maoni yanayotofautiana.

 Kauli za wabunge

Mbunge wa Manonga (CCM), Seif Khamis Gulamali amesema, “hakuna agenda nyingine, shughuli zilizopangwa kwa leo zimekwisha na kama unavyojua wizara hii huwa haina mambo mengi, mahusiano yetu yako sawa kwa hiyo hakuna tatizo.”

Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constantine Kanyasu amesema, “sijajua lakini nafikiri Dk Tulia ameona orodha ya wachangiaji  imekwisha, ndio maana akaongeza saa moja na akamaliza.”

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amesema, “tulijiandaa kushika vifungu na mpaka sasa hatujajua kwanini Bunge limemalizika muda huu maana mbunge aliyechangia kwa upande wa Chadema alikuwa mmoja tu ambaye ni Sugu (Joseph Mbilinyi-Mbeya Mjini).”

Nassari anaungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, “mimi mwenyewe sijui, sijui kuna nini. Nilijiandaa kukamata vifungu lakini imekwisha haraka haraka, hatujajua kuna nini.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga amesema Bunge si lazima kuahirishwa jioni, kwamba shughuli za siku husika zinapokwisha na vikao humalizika.

“Unajua hii wizara huwa si ngumu, ingekuwa wizara inayohusu mahindi au mifugo ungeona moto wake. Kwa hiyo Dk Tulia ameona wachangiaji wameisha akaona aliahirishe Bunge hadi kesho,” amesema mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda.

Mbunge wa Tanga Mjini (CUF), Mussa Mbarouk amesema, “mimi baada ya Naibu Spika kuongeza nusu saa, nikatoka kwenda msikitini lakini wakati narudi naambiwa limeahirishwa.”

“Unajua hii wizara ina mambo mengi tunajadili mustakabali wa Tanzania nje ya nchi, sasa kuijadili kwa muda mfupi sijajua kuna nini na sijajua kwa nini imepelekwa haraka haraka hivi.”