Bajeti ya Dk Mpango ni moto mitandaoni

Waziri wa Fedha, Philip Mpango

Muktasari:

Katika mitandao ya kijamii, hasa twittwer, wengi wamezungumzia kuhusu pendekezo la kuondolewa kwa kodi katika taulo za kike.


Dar es Salaam. Siku moja baada ya Waziri wa Fedha, Philip Mpango kuwasilisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19, wadau mbalimbali, wanasiasa na wananchi wa kawaida, wametoa maoni yao mitandaoni wakikosoa au kuisifia bajeti hiyo.

Katika mitandao ya kijamii, hasa twittwer, wengi wamezungumzia kuhusu pendekezo la kuondolewa kwa kodi katika taulo za kike.

Mkurugenzi wa Asasi ya kiraia ya Sikika, Irenei Kiria ameandika katika ukurasa wake wa twitter akisema:

“Nahisi tumefikia hatua sasa tunakopa ili tulipe deni (rob Peter to pay Paul) Mwaka wa fedha 2018/19 tutakopa 8.9Tri kwa masharti ya kibiashara lakini malipo ya deni la taifa kwa mwaka huo yatakuwa 10 trilioni. Yaani tutajazilizia ili tulipe deni.”

Mwanahabari, Carol Ndosi, yeye ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter akiipongeza serikali kwa kuondoa kodi kwenye taulo za kike:

“Kama Serikali imetusikia na kutoa tozo la kodi kwenye sanitary pads, inawezekana kabisa wakatusikiliza kwenye kubadilisha sheria na kuwaruhusu watoto wa kike kurudi shule pale wanapokua waathirika wa mimba za utotoni. Hili kundi linatuhitaji sana. Tumeshawaacha wangapi?”

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe, amesifu hatua hiyo ya serikali ya kuondoa kodi kwenye taulo za kike.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu yeye ameandika hivi:

“Tumedhamiria kuongeza uzalishaji wa ndani wa dawa. Hivi sasa asilimia 6 ya fedha za dawa ndio zinatumika kununua dawa, vifaa na vifaa tiba ndani ya nchi, ambacho ni kiwango cha chini sana ikilinganishwa na dawa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kwa gharama ya asilimia 94.”