Bajeti ya maendeleo, serikali yatoa theluthi moja

Muktasari:

Kuchelewa kutolewa kwa fedha hizo ikiwa imebaki miezi minne kwa bajeti hiyo kumalizika, kunatokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuchelewa kwa misaada na mikopo kutoka nchi wahisani.

Dodoma. Miradi mingi ya maendeleo nchini huenda ikakwama kutokana na Serikali kutoa theluthi moja tu ya fedha zilizotengwa kwa ajili hiyo katika bajeti yake ya mwaka 2016/17.

Kuchelewa kutolewa kwa fedha hizo ikiwa imebaki miezi minne kwa bajeti hiyo kumalizika, kunatokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuchelewa kwa misaada na mikopo kutoka nchi wahisani.

Wakati hali ikiwa hivyo, Serikali katika mwaka ujao wa fedha imepanga kukusanya na kutumia Sh31.6 trilioni ikilinganishwa na Sh29.5 trilioni za bajeti ya mwaka huu huku uwiano wa bajeti ya maendeleo ukishuka hadi kufikia asilimia 38 kutoka 40 ya mwaka huu.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwaeleza wabunge jana kuwa hadi Februari mwaka huu, fedha zilizokuwa zimetolewa kwa ajili ya maendeleo ni Sh3.97 trilioni kati ya Sh11.8trilioni zilizopitishwa na Bunge Juni, mwaka jana kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dk Mpango aliyekuwa akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa, Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/18, alisema fedha hizo zilizotolewa ni sawa na asilimia 34 ya zinazotakiwa hadi Juni. Fedha zilizotolewa zinajumuisha Sh871.8 bilioni kutoka nje.

Sababu za kukosa fedha

Akizungumzia sababu ya kukosa fedha Dk Mpango alisema, “Mojawapo ya mambo yaliyosababisha hali hii ni kuelekeza sehemu ya fedha za maendeleo kwenda kulipa madeni ya miradi ya maendeleo, lakini kiuandishi wa taarifa za bajeti zinahesabiwa upande wa matumizi ya kawaida.”

Dk Mpango alisema sababu nyingine ni kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo kutokana na majadiliano na washirika wa maendeleo kuchukua muda mrefu na pia kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la kimataifa.

Hata hivyo, alisema mwenendo wa kupungua kwa misaada na mikopo haipo kwa Tanzania pekee, bali nchi nyingine za Afrika zikiwamo Zambia, Algeria na Ivory Coast.

Serikali kukosa mkopo

Dk Mpango alisema Serikali imeshindwa kupata mkopo wa nje wenye masharti ya kibiashara katika bajeti ya mwaka 2016/17 kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri hasa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huo wa fedha. Katika kikao hicho kilichofanyika bungeni na kuongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha unaomalizika, Serikali ilipanga kukopa katika vyanzo vya kibiashara Sh2.1 tirioni ili kugharamia miradi ya maendeleo nchini.

Hata wakati wakipanga hivyo, alisema ndani ya kipindi hicho riba ilipaa kutoka wastani wa asilimia sita hadi asilimia tisa.

“Kutokana na sababu hiyo Serikali iliahirisha mchakato wa kukopa kutoka kwenye masoko hayo,” alisema.

Hata hivyo, Dk Mpango aliwaeleza wawakilishi hao kuwa gharama ya ukopaji katika masoko ya Ulaya imeanza kuimarika.

Alisema Serikali imeshasaini mkataba na Kuwait Fund wa Dola 51 milioni za Marekani kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chaya hadi Nyahua.

Pia, alisema Serikali itasaini hivi karibuni mkataba na Opec Fund wa Dola 18 milioni za Marekani na Abu Dhabi Fund For Development (ADFD) wa Dola 15 za Marekani kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Uvinza – Ilunde – Malagarasi.

Bajeti ya Sh31.6 trilioni

Dk Mpango alisema Serikali katika mwaka wa fedha 2017/18 inatarajiwa kukusanya na kutumia kiasi cha Sh31.6 trilioni.

Bajeti hiyo ni sawa na ongezeko la Sh2.6 trilioni ya bajeti iliyopitishwa na Bunge katika mwaka wa bajeti 2016/17.

Pia katika bajeti hiyo, fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka Sh11.8 trilioni bajeti ya mwaka 2016/17 hadi Sh11.9 trilioni mwaka 2017/2018 sawa na asilimia 38 ya bajeti yote inayopendekezwa.

Wahisani kuchangia asilimia 12

Dk Mpango alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh3.971.1 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 12.6 ya bajeti yote.

“Misaada na mikopo hii inajumuisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mifuko ya pamoja ya kisekta na kibajeti (GBS),” alisema.

Alisema Serikali inatarajia kukopa Sh6,156.7 bilioni kutoka soko la ndani na Sh4,948.2 bilioni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zilizoiva na Sh1208.4 bilioni sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Alisema ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa Sh1.595 trilioni kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.

Vipaumbele

Dk Mpango alitaja vipaumbele vya mpango huo kuwa ni ujenzi wa reli hususan kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (kilomita 205), kumpata mkandarasi wa kusanifu ujenzi kwa maeneo ya Morogoro hadi Makutopora (kilomita 336), Makutopora hadi Tabora (kilomita 294), Tabora hadi Isaka (kilomita 133) na Isaka hadi Mwanza (kilomita 249).

Pia kupata maeneo ya ardhi ya kuunganisha na kuanzisha treni kati ya Mpiji na Soga mkoani Pwani, Buhongwa (Mwanza) na Ihumwa Dodoma kwa ajili ya kituo kikubwa cha treni za mizigo na makasha.

Vipaumbe vingine ni kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kukamilisha ununuzi wa ndege tatu, mradi wa Liganga, makaa ya mawe Mchuchuma, kuanzisha kanda maalumu za kiuchumi, mradi wa Liquified Natural Gas, shamba la kilimo na sukari Mkulazi na kuhamishia shughuli za Serikali kuu Dodoma.

Changamoto za bajeti

Dk Mpango alisema changamoto za bajeti hiyo ni pamoja na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/2017 hadi kufikia Februari, mwamko mdogo wa kulipa kodi hususan kuzingatia matumizi ya mashine ya kielektroniki.

Alisema nyingine ni kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje na majadiliano ya muda mrefu yaliyosababisha kuchelewa kupatikana kwa fedha za washirika wa maendeleo.

Alisema Serikali itachukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kusimamia dhana ya kulipa kodi kwa hiari kupitia udhibiti wa matumizi ya EFD na kuendelea na majadiliano baina ya Serikali na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha fedha za misaada na mikopo nafuu zinapatikana kama zilivyoahidiwa.

Ndugai akerwa na ucheleweshaji

Awali, Spika wa Bunge Job Ndugai aliionya Serikali juu ya ucheleweshaji wa uwasilishaji wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa, kiwango na ukomo wa bajeti akisema kikanuni, unatakiwa kuwasilishwa Machi 11 ya kila mwaka.

“Kama ikiwa siku hiyo imeangukia siku siyo ya kazi basi uwasilishaji huu hufuatia siku inayofuata. Mkija mwakani namna hii haitawezekana, hatutakuwa na mjadala,” alisema Ndugai. Aliwataka mawaziri, makatibu wakuu, maofisa wa Serikali na wabunge, kuhakikisha wanakuwepo Dodoma kwa ajili ya uchambuzi wa mpango huo kisekta na kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakamilika kablaya kuanza kwa Mkutano wa Bunge Aprili 4.

Maoni ya wabunge

Wakizungumzia mpango huo, baadhi ya wabunge waliohojiwa walisema hawaoni jipya kwa sababu Serikali imetoa asilimia 34 tu ya fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu.

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde alisema ni vigumu kwa Serikali kutoa fedha zote zilizopitishwa katika bajeti.

“Hawawezi kumaliza (kutoa) kiasi kilichobaki katika kipindi cha robo mwaka kilichobaki, kwa hiyo hapa hakuna jipya,” alisema Silinde ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.

Alisema kwa mwezi, Serikali imekuwa ikikusanya wastani wa Sh1 trilioni na Sh570 bilioni hutumika kulipa mishahara ya watumishi wa umma huku kiasi kilichobaki kikienda kulipa madeni.

Mbunge wa Kerwa (CCM), Innocent Bilakwate alisema Serikali imeweka jitihada nzuri katika ujenzi wa miundombinu nchini lakini sasa ni lazima iangalie Watanzania wengi wanajishughulisha na nini na kujikita katika kuwainua.

“Asilimia zaidi ya 70 wanajishughulisha na kilimo na ufugaji, tunatakiwa tujikite hapo katika kuwainua kiuchumi. Kuangalia viwanda vidogovidogo vya kuchakata mazao ya wakulima ni eneo jingine la kujikita,” alisema.

Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe alisema bajeti hiyo haielezi jinsi malengo yaliyopangwa yatakavyotekelezwa. “Kwa mfano tunasema tunajenga uchumi wa viwanda lakini bajeti haisemi tunajengaje jengaje huo uchumi.”

Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge alisema mapendekezo ya mpango huo yanatoa matumaini kwa Watanzania.

Mbali ya wabunge, baadhi ya wasomi pia walihojiwa. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Omari Mbura alisema utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha ulikuwa una shaka baada ya Serikali kuweka kiasi kikubwa kwenye miradi ya maendeleo kwa kupunguza matumizi ya kawaida.

“Upunguzaji uliofanywa inawezekana ulielekezwa kwenye maeneo muhimu kama vile ongezeko la mishahara na utekelezaji wa miradi ambayo haikuwamo kwenye bajeti husika. Lakini, huenda kiasi hicho kikaongezeka, kuna miezi minne mbele,” alisema Dk Mbura.

Alitoa mfano wa ujenzi wa hosteli za UDSM na nyumba za Jeshi la Magereza kwamba ni miradi ambayo haikuwamo kwenye bajeti ya mwaka huu.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara, Dk Haji Semboja alisema ni kawaida kwa bajeti ya kwanza kwa kila Serikali mpya kuwa na changamoto ambazo zinaweza kuepukwa kwa kuweka ukuaji mdogo kutoka kwenye ile waliyoikuta.

“Nilikuwa nategemea bajeti ya kwanza iwe ya mpito. Hii ya mwaka huu Serikali itakuwa na picha kamili ya inachotakiwa kufanya. Tunahitaji physical displine; tukusanye na kutumia tulichopanga. Serikali ilitarajia kiasi kikubwa kuliko uwezo wa TRA kukusanya,” alisema Dk Semboja.