Bakwata wamshukuru Rais Magufuli

Muktasari:

Jana Rais Magufuli alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa msikiti mkuu wa Baraza hilo 

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limemshukurua Rais John Magufuli kwa umakini wake katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili baraza hilo.

Jana Rais Magufuli alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa msikiti mkuu wa Baraza hilo na  kuchangia Sh10 milioni kwa ajili ya ununuzi wa saruji  kwa lengo la kuharakisha ujenzi wa msikiti huo.

Msikiti huo una ukikamilika, utakuwa na uwezo wa  kuchukua zaidi ya waumini 6,000 .

Msikiti huo uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam unajengwa kwa ufadhili wa Mfalme Mohamed VI wa Morocco baada ya Rais Magufuli kumuomba awajengee waislamu.

Akizungumza na wanahabari   leo Juni 13, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Hamis Mataka amesema Waislamu  wameridhika na ufuatiliaji huo.

 “Jana alifanya ziara ya kushtukiza katika msikiti huo na kwa kuonyesha umuhimu wa ujenzi huo alitoa mchango wake hivyo kwa niaba ya Waislamu wote Bakwata tunatoa shukrani zetu za pekee kwa Rais Magufuli,”amesema.

Akielezea msikiti huo utakavyokuwa amesema mbali na uwezo wa kuchukua zaidi ya waumini 6,000 utakuwa pia na ofisi ya kufanyia mikutano itakayochukua watu 300 pamoja na maktaba.

Pia, Mataka alitoa shukrani zake kwa Balozi wa Morocco nchini Abdelilah Benryane kwa ushirikiano wake wa karibu kwa Bakwata katika kusimamia shughuli mbalimbali ikiwamo ujenzi wa msikiti huo.