Bakwata yadaiwa mamilioni na watumishi

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Hamis Mataka akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.kulia ni Sheikh, Hassani Chizenga mkurugenzi kitengo cha  Dawa na  Tbligh Tanzania .Picha na Omar Fungo

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata na msemaji wa baraza hilo, Sheikh Khamis Mataka aliwaambia wanahabari Dar es Salaam jana kuwa changamoto ya kutolipwa watumishi wa Bakwata kwa muda mrefu ni kutokana na matatizo ya kifedha yaliyotokea miaka ya nyuma ambayo sasa yanatatuliwa kwa kufanyika marekebisho ya kimfumo katika uendeshaji.

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) linadaiwa Sh176 milioni na watumishi wake na kuahidi kuwa litaanza kulipa madeni hayo mwishoni mwa mwezi huu.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata na msemaji wa baraza hilo, Sheikh Khamis Mataka aliwaambia wanahabari Dar es Salaam jana kuwa changamoto ya kutolipwa watumishi wa Bakwata kwa muda mrefu ni kutokana na matatizo ya kifedha yaliyotokea miaka ya nyuma ambayo sasa yanatatuliwa kwa kufanyika marekebisho ya kimfumo katika uendeshaji.

“Jumla ya madai ya wafanyakazi wa Bakwata makao makuu ni Sh176 milioni mpaka sasa, uongozi umekuwa ukiwaeleza hali halisi wafanyakazi na tuna uhakika wa kuanza kulipa mwishoni mwa mwezi huu Inshaallah,” alisema Sheikh Mataka.

Alisema madeni hayo ni ya muda mrefu ambayo Mufti Abubakary Zubeir ameyakuta na kwamba yalitokana na kutokuwapo kwa mfumo mzuri wa udhibiti na kutokaguliwa kwa hesabu za mapato na matumizi ya Baraza kwa miaka sita.

“Kwa utaratibu mpya uliowekwa na uongozi wa sasa lazima Baraza liwe na bajeti ya kila mwaka, na fedha zote zitatoka kulingana na mipango ya bajeti na zitatumika kwa maandishi,” alisema.

Alisema hatua hiyo ya mabadiliko ya kimfumo haijawafurahisha baadhi ya watu ambao wameanza kueneza uvumi na uongo kwa lengo la kuvuruga taswira ya uongozi wa baraza hilo.

Alisema watu hao wamekuwa wakieneza taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa wafanyakazi wa Baraza hawajalipwa mishahara, Mufti amejimilikisha shule 10 za baraza hilo na kuna njama za kumuondoa madarakani.

Sheikh Mataka alisema habari hizo ni za uongo na nia yake ni ovu ukiachilia mbali hilo la wafanyakazi kutolipwa mishahara ambalo ni la kweli.

“Ni muhimu wananchi wakatumia vyema neema ya maendeleo ya kiteknolojia badala ya kuitumia vibaya kwa kuvunja heshima za watu kwa madai ya uongo na kueneza fitina. Baraza kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanalifuatilia kwa karibu,” alisema.

Mkurugenzi wa Daawa na Tabligh wa Bakwata, Sheikh Hassan Chizenga aliwataka wananchi kuwa makini na matamshi yao na kutumia ndimi vizuri kwa kuwa siku ya hukumu kila neno litahesabiwa.