Balozi Kijazi awapa somo makatibu wakuu, Ma - RAS

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi

Muktasari:

  • Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Kijazi akizungumza na makatibu wakuu,  katibu tawala (RAS) amewataka kuzingatia sheria, kanuni na miongozo pindi wanapofanya uamuzi

Dodoma. Serikali imewataka makatibu wakuu kuhakikisha wanatekeleza muundo mpya wa utekelezaji wa shughuli za wizara zote ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama zisizo za lazima.

 Hayo yamesemwa leo Septemba 19, 2018 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi

Alipokuwa akizungumza katika mkutano wa siku tatu unaowashirikisha makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu na makatibu tawala wa mikoa nchini uliofanyika jijini Dodoma.

 Amesema mkutano huo wa aina hiyo ni wa kwanza kufanyika tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, walipokutana mara ya mwisho mwaka 2015 walikuwa wajumbe 63, lakini leo kati ya hao waliobakia katika nafasi hizo ni 15.

 Amesema kwa idadi hiyo, asilimia 81 ni wateule wapya na kwamba lengo la mikutano hiyo ni kujadiliana, kubadilishana maarifa na uzoefu.

 “Mikutano hii hutusaidia sisi wajumbe kufahamiana zaidi, kujenga mahusiano mema ya kikazi baina yetu yenye lengo la kufanya kazi kama timu moja ya kuwahudumia wananchi,” amesema.

 Amesema umuhimu wa mikutano ni mkubwa mno na kuwahakikishia mikutano kama hiyo itakuwa ikifanyika kila mwaka baada ya kutofanyika kwa miaka miwili mfululizo.

 Balozi Kijazi amesema mikutano hiyo ilishindwa kufanyika kwa miaka miwili mfululizo kutokana na shughuli ya kupanga upya safu ya uongozi katika Serikali na taasisi zake pamoja na kuboresha mifumo mbalimbali ya uendeshaji wa Serikali.

 Amesema wameandaa muundo mpya wa jinsi ya kutekeleza shughuli katika wizara zote isipokuwa Ofisi ya Rais ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), lengo ni kuongeza ufanisi na kuondoa gharama kwa Serikali zisizo za lazima.

 “Ninawakumbusha makatibu wakuu tena, ni jukumu lenu kuhakikisha miundo hii inatekelezwa isije ikapita tena mwaka ipo katika ma-shelve, bado mnaendelea na ‘structure’ ambayo mlikuwa nayo kule nyuma. Investment kubwa sana imefanyika mpaka kufikia hatua hii,” amesema.

 Amewaonya wasije wakafika mahali wakaacha kuitekeleza wakati tayari Serikali na Rais John Magufuli ameshaiidhinisha miundo hiyo.

 “Natambua mnavyojituma katika nafasi zenu na napenda kuwapongeza sana na kuwahimiza kuendelea na uwajibikaji huo bila kutetereka wala kurudi nyumba. “Mkumbuke nafasi zenu ni za uamuzi na msipofanya uamuzi sahihi na kwa wakati katika maeneo yenu, mtakwamisha upatikanaji wa maendeleo na huduma muhimu,” amesema.

 Amewakumbusha wanapofanya uamuzi ni lazima yazingatie sheria, kanuni, miongozo na taratibu zinazoongoza maeneo wanayoyasimamia.

 Amesema zipo baadhi ya taasisi ambazo zimekamilisha na kuidhinisha miundo yake lakini zipo taasisi zaidi ya 400 bado hazijakamilisha na kwamba kazi hiyo inaendelea na wana aamini kabla ya katikati ya mwaka ujao kila wizara na taasisi itakuwa na muundo ambao Serikali ya awamu ya tano inaamini ni sahihi.

 “Lakini katika uamuzi tunaoufanya ni lazima tuzingatie uzalendo na maslahi ya Taifa. Tusiweke ubinafsi wetu mbele kwa sababu wengi ndipo wanapoharibikiwa hapo. Anadhani kupata nafasi hii ni nafasi ya kuneemeka ama kunyoosha maslahi yake sivyo, wewe ni mtumishi wa umma,” alisema.

Mwisho