Balozi Kijazi awataka Watanzania kupima afya zao

Balozi John Kijazi 

Muktasari:

Balozi Kijazi amesema ni muhimu kufanya vipimo mara kwa mara na kama ikitokea umebainika kuwa na ugonjwa inakuwa rahisi kuupatia tiba wakati ugonjwa huo ukiwa kwenye hatua za awali.

Dar es Salaam. Watanzania wametakiwa kujiwekea utaratibu wa kuangalia afya zao mara kwa mara ili kuhakikisha wakati wote afya zinakuwa salama.

Rai hiyo imetolewa  leo Jumatatu, Julai 17 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akiwa ni mmoja wa waombolezaji waliofika kwenye msiba wa mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Linah Mwakyembe aliyefariki dunia juzi usiku kutokana na ugonjwa wa saratani ya titi.

Sanjari na hilo, Balozi Kijazi amewasisitiza Watanzania kuwa na utamaduni  wa kufanya mazoezi ili kujiweka mbali na magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema Watanzania wengi wanapoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo saratani.

"Ni muhimu kufanya vipimo mara kwa mara, ikitokea umebainika kuwa na ugonjwa ni rahisi kuupatia matibabu ukiwa kwenye hatua za awali," amesema.

"Tatizo linapogundulika mapema ni rahisi kuokoa maisha ya mgonjwa tena kwa gharama nafuu za matibabu kinyume na hapo gharama zinakuwa juu na kupona inakuwa bahati," amesisitiza.