Wanafunzi 24 wapata udhamini wa masomo UDSM

Muktasari:

Barclays itatumia Sh70 milioni kugharimia masomo ya wanafunzi 24.

Dar es Salaam. Benki ya Barclays Tanzania imetoa vyeti kwa wanafunzi 24 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) walioshinda shindano la udhamini wa masomo liitwalo 'balozi mwanafunzi'.

Akizungumza wakati wa utoaji wa vyeti hivyo leo Jumanne Desemba 12,2017, mkurugenzi wa benki hiyo, Abdi Mohamed amesema sekta binafsi ni muhimu kuwekeza katika ukuzaji wa elimu ambao matokeo yake ni uzalishaji mkubwa.

"Uwepo wa maarifa katika jamii ni nyenzo katika ukuzaji wa uchumi na maendeleo ya nchi, nasi tunawajibika kuendeleza jamii ya Watanzania," amesema Mohamed.

Amesema katika mradi wa kuwasomesha wanafunzi mwaka huu wa masomo, benki itatumia Sh70 milioni na itaendelea kuwahudumia wanafunzi hao hadi watakapomaliza masomo yao.

"Wanafunzi wote 24 waliopata ufadhili huu tutawalipia gharama zote za masomo. Kuna ambao wapo mwaka wa kwanza, wengine mwaka wa pili na mmoja ni wa mwaka wa tatu," amesema Mohammed.

Amesema wameanza kwa wanafunzi wa UDSM na wanatarajia kuangalia uwezekano wa kushirikiana na vyuo vingine.

Makamu Mkuu wa Chuo cha UDSM (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa aliyekuwepo katika hafla hiyo amesema Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) haiwezi kutosheleza mahitaji ya wanafunzi wote, hivyo wadau wa sekta binafsi wanapaswa kusaidia.

"UDSM tunachukua wanafunzi waliopata ufaulu mzuri lakini jambo la kusikitisha ni kwamba baadhi yao hushindwa kuendelea na masomo hasa pale wanapokosa mkopo, wanashindwa kumudu gharama hivyo wakipata ufadhili ni neema kwao," amesema.