Basata, Roma wavurugana

Roma Mkatoliki

Muktasari:

Stamina mmoja wa wasanii wanaounda kundi hilo alichapisha barua ya wito kutoka Basata inayowataka wafike kuujadili wimbo wao mpya, Parapanda baada ya Baraza hilo kudai kuwa halijawaita.


Baraza la Sanaa la Taifa(Basata), limesema halijawaita wala kufungia wimbo wa Parapanda ulioimbwa na wasanii wa kundi la Rostam, Roma Mkatoliki na Stamina na kusema kuwa labda wameamua kujifungia wenyewe kwa lengo la kutafuta ‘kiki’.

Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Roma kupitia ukurasa wake wa Instagram kuandika maneno ya kuilaumu Basata kwamba inaua vipaji na ubunifu wa wasanii na kuhoji wimbo wao huo una tatizo gani.

Akilizungumzia hilo, Katibu wa Baraza la Sanaa, Godfrey Mngereza, amesema hawajaufungia wimbo huo na haujapitishwa mikononi mwao hadi sasa kwa ajili ya kuhaririwa.

Hata hivyo, Stamina mmoja wa wasanii wanaounda kundi hilo alichapisha barua ya wito kutoka Basata inayowataka wafike kuujadili wimbo wao mpya, Parapanda baada ya Baraza hilo kudai kuwa halijawaita.