Bashe kukumbana na vigingi vitatu

Muktasari:

  • Katika hoja hiyo inayogusia matukio ya mashambulio ya risasi, kusinyaa kwa demokrasia nchini, utekaji, watu kupotea na mauaji ambayo pia yanawahusisha wanasiasa, Bashe atalazimika kutumia nguvu kubwa kushawishi ili ijadiliwe bungeni, hatimaye kuridhiwa na idadi kubwa ya wabunge.

Dar/Dodoma. Siku tatu baada ya mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe kuwasilisha katika ofisi ya Bunge hoja yake binafsi iliyobeba mambo manane, huenda akakumbana na vigingi vitatu kutoka ndani ya chama chake, wabunge wenzake na katibu wa Bunge.

Katika hoja hiyo inayogusia matukio ya mashambulio ya risasi, kusinyaa kwa demokrasia nchini, utekaji, watu kupotea na mauaji ambayo pia yanawahusisha wanasiasa, Bashe atalazimika kutumia nguvu kubwa kushawishi ili ijadiliwe bungeni, hatimaye kuridhiwa na idadi kubwa ya wabunge.

Machi 5, mbunge huyo aliwasilisha hoja hiyo kwa Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai ambaye alikiri kuipokea na jana wabunge zaidi wa chama tawala, Nape Nnauye (Mtama) na Livingstone Lusinde wa Mtera walimuunga mkono.

Vigingi

Bashe atalazimika kumwandikia barua katibu wa wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza kueleza hoja yake hiyo ambaye anaweza kufikisha suala hilo kwa kamati ya uongozi ya wabunge wa chama hicho inayohusisha wenyeviti wa kamati za Bunge wanaotokana na CCM.

Pili, ataipeleka kwa katibu wa Bunge ambaye ataipitia kuona kama imekidhi kanuni za Bunge na kama itakuwa na upungufu huenda akatakiwa kuirekebisha na hata akiipitisha, lazima Spika wa Bunge aione na kuikubali.

Tatu, ikishapita maeneo hayo yote, ataiwasilisha bungeni, kujadiliwa na wabunge na ili ilidhiwe, inatakiwa iungwe mkono na wabunge wengi kati ya 393 waliopo na ili ipite, ni lazima iungwe mkono na pengine nusu ya idadi hiyo kama wote watakuwapo bungeni siku husika.

Apangua vigingi

Akizungumzia vigingi hivyo, Bashe alisema,” Ninachopaswa kufanya ni kumwandikia barua katibu wa wabunge wa CCM kuhusu hoja yangu na atanijibu kwa barua. Vyovyote atakavyonijibu, nikiandaa hoja yangu naye nitampelekea na atatoa maelekezo.

“Anaweza kutoa maelekezo kuwa hoja yangu iende kwenye kamati ya uongozi ya CCM.”

Alipoulizwa haoni kama hoja hiyo inaweza kupanguliwa na katibu wa Bunge alisema, “Aaaah, katibu anapaswa kuangalia kama nimefuata kanuni za Bunge, kama ina upungufu atanijibu nitaiweka sawa.”

Kuhusu idadi ya wabunge wanaopaswa kuiunga mkono hoja yake, alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge inayotaka hoja binafsi kuungwa mkono na wabunge wengi alisema, “Hakuna idadi ya namba kwamba lazima uungwe mkono na wabunge kiasi fulani. Wengi wakikuunga mkono hoja inapita.

“Kwa sasa kuna wabunge zaidi ya 300. Suala la idadi ya wabunge huangaliwa zaidi kama wabunge wanabadilisha Katiba ya nchi au kupitisha bajeti.”

Rweikiza amjibu

Rweikiza ambaye ni mbunge wa Bukoba Vijijini alipoulizwa kuhusu hoja hiyo ya Bashe, alisema, “Nitaitazama nikiridhika nayo nitaipeleka hatua nyingine ambayo ni kwa Spika wa Bunge. Kwa sasa nipo Bukoba bado sijaiona hoja yenyewe.”

Nape amuunga mkono

Nape jana alizungumza na Mwananchi na kuunga mkono hoja ya Bashe kwamba moja ya kazi ya mbunge ni kuchukua mambo yanayozungumzwa katika jamii na kuleta utata na kuyapatia suluhisho kwa kutumia chombo kilichowekwa kikatiba.

“Mfano leo ukiwachukua Watanzania 10 ukiwaambia wazungumze hoja ambayo inasumbua vichwa vyao, suala la ulinzi na usalama kwao nadhani linaweza kuwa namba moja. Kila mtu ukikutana naye atakwambia habari ya watu wasiojulikana, hofu, watu kupotea,” alisema Nape.

Alisema hoja ya Bashe imegusa makundi mengi katika jamii kwa maelezo kuwa imebeba hadi matukio yaliyowahi kuwakumba wanasiasa bila kujali itikadi zao na viongozi wa dini.

“Ni busara kumuunga mkono na kupitia njia hiyo itasaidia ukweli kujulikana. Kifupi naunga mkono hoja ya Bashe. Kumekuwa hakuna majibu ya kuridhisha kila wakati jambo hili linapotokea. Kila mara tutaambiwa uchunguzi unaendelea watu hawajulikani lakini matukio yanaendelea kutokea. Tumeona Kibiti yametokea mambo makubwa na Dar es Salaam watu wameokotwa baharini,” alisema.

Nape pia alitolea mfano tukio la yeye kutolewa bastola hadharani na mtu aliyeelezwa kuwa si askari wa Jeshi la Polisi, katika eneo ambalo polisi walikuwapo na mtu huyo hajakamatwa hadi leo.

Kwa upande wake, Lusinde alisema kuunga mkono au kutounga mkono hoja ya Bashe, kutategemea na ushawishi atakaoutoa.

“Hoja hiyo nimeisikia, kwa kweli ni nzuri sana lakini kumuunga mkono ni kutegemea ushawishi wake, ila ingenoga kama tungeanza nayo kwenye vikao vya chama na kujipanga vizuri zaidi,” alisema Lusinde.

Msekwa atia neno

Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema, “Bado hajaiwasilisha licha ya kuwa ameshaeleza mambo kadhaa. Subiri kwanza, msitake kuwahisha mambo. Ngoja aiwasilishe tusikie nini kitazungumzwa.”

Hoja Binafsi za Bashe

1. Kusinyaa kwa demokrasia na haki za raia

2. Kupotea, kutekwa na kuuawa kwa raia katika chaguzi

3. Kupigwa risasi na kuumizwa raia na kikundi ambacho kinaitwa “wasiojulikana”

4. Mauaji ya viongozi wa kisiasa wanaotokana na vyama halali vya siasa nchini

5. Ukandamizwaji wa uhuru wa raia kutoa maoni, kukosoa na kushauri

6. Matumizi mabaya ya sheria na ukandamizaji wa demokrasia ndani ya nchi

7. Haki za kikatiba na kisheria za vyama vya siasa kutoheshimiwa

8. Tuhuma dhidi ya vyombo vya usalama na matumizi ya silaha za moto kwa raia