Bashiru Ally awashukia wanaodai CCM inawanunua wapinzani

Muktasari:

  • Dk Bashiru amesema CCM hakiwezi kununua madiwani na wabunge wa vyama vya upinzani kwa kuwa chama hicho tawala kipo makini na hakiendeshwi  kama taasisi ya mtu binafsi

Liwale.  Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru  Ally  amewataka wanasiasa  kuachana na maneno kuwa chama hicho tawala kinawanunua madiwani na wabunge wa vyama vya upinzani ili kuviua.

Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Septemba 25, 2018 katika uzinduzi wa kampeni za  ubunge wa Liwale na  udiwani wa  Kibutuka  wilayani  humo mkoani Lindi.

Amesema yeye  ni katibu mkuu wa CCM na ndio  msimamizi  mkuu wa  mali  za chama, hivyo hawezi kuidhinisha fedha kwa ajili ya kuwanunua wapinzani kwa maelezo kuwa mikono yake iko safi.

“Habari  kuwa tunanunua wapinzani  si kweli. Siwezi kutoa fedha za chama kufanya hivyo. Wanaotoa kauli hizo wanakikashifu chama na mimi binafsi. Wakome,” amesema.

Amebainisha kuwa CCM ni chama makini si legelege kama vyama vingine vinavyokufa kutokana na viongozi wake wa juu   kuwagawanya wanachama, sambamba na kuendeshwa kwa makundi.

Amesema chama tawala kinaendelea kutamba kwa sababu Watanzania hawapo tayari kuvikumbatia vyama vya upinzani vinavyoendeshwa kama kampuni ya mtu binafsi.

“Watanzania wanahitaji vyama vinavyoengeshwa kitaasisi na vyenye muundo, falsafa, itikadi  na sera nzuri  ya kuwaletea maendeleo. Vyama hivyo havipo nchini zaidi ya CCM,” amesema.