Bawacha wasema katazo la mikutano ya hadhara ni mwiba kwa wanawake

Muktasari:

  • Wasema uamuzi huo unaminya juhudi za wanawake kufikia usawa wa asilimia 50 kwa wanawake na wanaume

Dodoma. Baraza la Wanawake  Chadema (Bawacha) limesema uamuzi wa Serikali kupiga marufuku mikutano ya hadhara unarudisha nyuma juhudi za wanawake kufikia usawa wa asilimia 50 kwa wanawake kwa wanaume.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Juni 24, 2018 na makamu mwenyekiti wa baraza hilo, Hawa Mwaifunga wakati akizungumza na wanahabari katika mkutano wa kamati ya utendaji ya baraza hilo uliofanyika mjini hapa.

Mkutano huo wa siku mbili pamoja na mambo mengine unalenga kuwapa mafunzo, mbinu na ujasiri viongozi wa mikoa wa chama hicho.

Mwaifunga amesema wanawake wengi wamekuwa na hofu kutokana na uamuzi wa kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara, jambo ambalo linawafanya wanawake washindwe kujitosa katika siasa.

Amesema uamuzi huo umewanyima fursa Watanzania kuwasikiliza wanasiasa ili baadaye waje wafanye uamuzi wa kuwachagua wagombea wa chama kinachofaa.

“Kwa sasa ni kutishana na kukamatwa na kuwekwa ndani. Kipindi cha nyuma watu walifanya siasa za kistaarabu sana, ndiyo maana tuliwapata akina Halima Mdee (mwenyekiti Bawacha), Paulin Gekul (Babati Mjini (Chadema). Walipatikana baada ya kuonekana majukwaani,” amesema.

Katibu wa Bawacha,  Grace Tendega amesema wataendelea kupambana  licha ya kuwa wanaoonekana kufanya siasa majukwaani wanakamatwa.

Amesema baraza hilo limejipanga kuhakikisha majimbo sita yanayoongozwa na wabunge wanawake wa Chadema yanalindwa.

Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Songwe, Sophia Mwabenga amesema mafunzo waliyopewa yatawasaidia kufanya siasa bila kuogopa chochote.