Kamanda wa Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro

Muktasari:

Vijana hao, wanadaiwa kuwarubuni wasichana kuwa watawafundisha kuogelea lakini baadaye huwalazimisha kufanya ngono wakiwa majini.

Dar es Salaam. Polisi jijini Dar es Salaam wamewakamata watu 33 wakiwamo vijana wanaopenda kukaa ufukweni maarufu ‘beach boys’ kwa tuhuma za kuwahadaa wasichana kimapenzi.

Vijana hao, wanadaiwa kuwarubuni wasichana kuwa watawafundisha kuogelea lakini baadaye huwalazimisha kufanya ngono wakiwa majini.

 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema  watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya askari kufanya msako na kukutwa wakifanya mapenzi kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi.

 Sirro amesema  jeshi hilo lilifanya doria kwa kutumia askari kanzu, mbwa na farasi kwenye fukwe hiyo.

“Msako huo pia ulifanywa na askari waliovalia sare, walizunguka maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye fukwe ili kuhakikisha hali inakuwa shwari,” amesema Sirro na kuongeza:

“Beach boys’ wanapofika kwenye kina kirefu majini hutumia mbinu ya kutaka kuwatosa watu hao kwenye maji huku wakiwalazimisha kufanya nao mapenzi kwa lazima”.