Beatrice mjasiriamali anayepambana na mbu wa malaria

Muktasari:

  • Ipo mishumaa inayofukuza mbu wasumbufu hasa waenezao maralia ambao ni miongoni mwa maradhi yanayoongoza kwa kusababisha vifo kwa watu wengi nchini.

Mara nyingi watu waishio mjini huwasha mshumaa pale umeme unapokata lakini wengi hawajui kuwa kuna baadhi ya mishumaa yenye kazi maalumu ambayo huwashwa hata kama umeme upo.

Ipo mishumaa inayofukuza mbu wasumbufu hasa waenezao maralia ambao ni miongoni mwa maradhi yanayoongoza kwa kusababisha vifo kwa watu wengi nchini.

Licha ya wengi kutolifahamu hili, Beatrice Mkama (38) ni mjasiriamali aliyeiona na kuamua kuichukulia kama fursa ya kujiingizia kipato.

Anasema alipata maarifa ya utengenezaji wa mishumaa hiyo kutoka Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (Sido) mwaka jana na kuongeza ujuzi kutoka kwa wajasiriamali wazoefu.

“Mimi ni (katibu muhtasi) secretary katika ofisi ya wakili wa kujitegemea lakini huwa natumia muda wangu wa ziada kuhakikisha kuwa najiongezea kipato,” anasema Beatrice

Anasema alianza kwa mtaji wa Sh40,000 kuanzisha biashara hiyo na kuisimamia kikamilifu kuhakikisha inakua na kufika mbali. Anasema huwa anatengeneza mishumaa 100 kwa siku anayoiuza Sh1,000 kila mmoja. Yeye huiuza kwa wafanyabiashara wa rejareja waliopo maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam anaoweza kuwafikia kwa haraka na urahisi.

“Haikuwa rahisi kuwaaminisha watu juu ya kile nachofanya. Wapo waliokuwa wanafikiri kuwa mishumaa hii inaua mbu hivyo unapowaambia inafukuza tu wanakosa uaminifu na wanahisi wanadanganywa,” anasema Beatrice.

Wakati anaanza kufanya uzalishaji w amishumaa hiyo, anasema alikuwa anaamini ipo siku biashara hiyo itamlipa lakini hakujua kama soko la bidhaa hilo litakuwa kubwa zaidi ya alivyofikiri.

“Kutokana na kuitangaza kupitia mitandao ya kijamii nimekuwa nikipata oda nyingi ambazo wakati mwingine nashindwa kuzitimiza kutokana na mtaji wangu kuwa mdogo,” anasema Beatrice.

Anasema kuna wateja wengi wanaopatikana mikoani wanaohitaji bidhaa hiyo lakini anashindwa kuwafikishia kutokana na kukosa wakala na baadhi ya wateja kuagiza mishumaa michache.

Anasema ni changamoto kusafirisha mishumaa michache ambayo huombwa na wateja walio maeneo tofauti nchini kwani gharama za usafirishaji ni kubwa. Kutokidhi mahitaji ya wateja wake wadogo waliopo mikoani ni miongoni mwa changamoto anazozifanyia kazi kuhakikisha anaongeza ushawishi wake kwao.

Anayo mashine ndogo anayoitumia kuzalisha mishumaa hiyo lakini mpango alionao ni kupata mashine kubwa zaidi ili kukuza biashara yake.

“Nikiwa na mashine kubwa nitakuwa na uwezo wa kuzalisha hadi mishumaa 300 kwa siku kwa sababu yenyewe haihitaji kupoza bali unachanganya kila kitu na kuweka na mashine inafyatua mishumaa,” anasema Beatrice.

Anaamini mtu yeyote anayefanya biashara ana nafasi kubwa ya kufanikiwa ikiwa ataongeza ubunifu kidogo kwa sababu itakuwa chachu ya kuwavutia wateja wake na kuwafanya wapende kutumia bidhaa zake.