VIDEO-Bei ya nyanya haishikiki kila kona

Mchuuzi wa nyanya katika Soko Kuu la jijini Mwanza,  Devotha Nkungu akipanga mafungu bidhaa hiyo sokoni hapo. Bei ya nyanya imepanda kwa sasa analazimika kuuza Sh 3,000 kwa fungu moja badala ya Sh1,000 ya awali. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

  • Wafanyabiashara wasema bei ya nyanya imepanda kutokana na mavuno kupungua mwaka huu

 Nyanya sasa ni dili. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na bei ya bidhaa hiyo kutoshikika huku mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zikitajwa kuwa chanzo cha kuadimika huko.

Bei hiyo imepanda katika baadhi ya masoko ambayo Gazeti la Mwananchi lilitembelea juzi, yakiwamo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara na Kagera.

Bei ya sado moja ya nyanya katika masoko mbalimbali ya mikoa hiyo ni kati ya Sh7,000 na 10,000, ikiwa ni ongezeko la takribani Sh3,000 huku kasha kubwa la nyanya zenye ubora likiuzwa kwa Sh70,000 hadi 100,000.

Pwani

Katika masoko ya wilaya za Kibaha, Chalinze na Bagamoyo nyanya zimepanda kutoka Sh5,000 kwa sado moja hadi Sh9,000 huku fungu la nyanya tatu badala ya tano likiuzwa kwa Sh500.

Mfanyabiashara wa Soko la Chalinze, Shukuru Dulla alisema bei imepanda kwa sababu upatikanaji wa nyanya shambani umekuwa mgumu kwa kuwa nyingi zinaoza kwa sababu ya mvua kunyesha.

“Hata bei iliyopo sasa inaweza kupanda kwa sababu nyanya hazipatikani maeneo jirani. Tulikuwa tunazifuata Morogoro, Ruvu na Iringa ambako pia hazipatikani na sasa tunalazimika kuzifuata Kahama na Shinyanga,” alisema Mwanaheri Saidi, mfanyabiashara wa Soko la Kwa Mathias, Kibaha.

Dar es Salaam

Soko la Buguruni, bei ya nyanya kwa kasha moja ni Sh39,000 hadi Sh80,000 kulingana na ubora, huku sado moja ikiuzwa kati ya Sh8,000 na Sh9,000.

Katika soko la Mabibo, kasha moja la nyanya linauzwa kwa Sh90,000 huku nyanya moja ikiuzwa kati ya Sh150 na Sh300.

Wauzaji wa rejareja katika Soko Dogo la Kijichi, wanauza nyanya moja kwa kati ya Sh200 na Sh300 na fungu moja la nyanya nne ndogo ndogo linauzwa kwa Sh1,000.

Mwenyekiti wa Soko la Temeke Stereo, Rajabu Kingalu alikiri kuwapo kwa uhaba wa nyanya sokoni hapo.

Alisema uhaba huo ndiyo unasababisha kupanda kwa bei hasa zinazotoka Zanzibar ambazo makasha yake ni makubwa na huuzwa kwa Sh90,000 hadi Sh100,000.

“Lakini nyanya za kutoka Iringa na kwingine Tanzania Bara bei yake ni kuanzia Sh450 hadi 500 (kwa nyanya moja) ambayo bado ni kubwa ukilinganisha na Sh200 hadi 250 ya awali.

“Mvua ndiyo zimesababisha shambani vitu vinaharibike zikiwamo nyanya ambazo zinazokuja nyingine hazina ubora,” alisema Kingalu.

Gazeti la Mwananchi lilitembelea Soko la Temeke Stereo na kukuta sado moja ya nyanya ikiuzwa kati ya Sh8,000 na Sh9,000 kulingana na ubora wa nyanya.

Mchuuzi wa nyanya katika Soko la Temeke Stereo, Vaileth Shao alisema anawahurumia wachuuzi wa mitaani ambao wananunua sado ya nyanya sokoni hapo kwa Sh9,000.

“Nikitafakari naona na wao wanafanya biashara kwa mazoea, lakini siyo kwa ajili ya kupata faida, kwa sababu sisi wenyewe pamoja na kuuza bei hiyo hatupati kitu,” alisema Shao.

Mfanyabiashara wa nyanya katika Soko la Kariakoo, Faraja Kihwelo alisema hali ya upatikanaji wa bidhaa hiyo imekuwa mbaya.

Kihwelo alisema awali, walikuwa wananunua nyanya kutoka Zanzibar kasha moja kwa Sh85,000 hadi Sh90,000 lakini juzi ilikuwa ni Sh100,000.

“Nyanya za Iringa bei yake imefikia Sh50,000 kwa kasha na kibaya zaidi zinawekwa zikiwa chafu na haziwezi kudumu kwa sababu zimepigwa sana mvua,” alisema Kihwelo.

Kanda ya Ziwa

Jijini Mwanza nyanya zimepanda kutoka Sh4,000 hadi Sh8,000 kwa sado moja.

Mfanyabiashara wa bidhaa hiyo katika Soko Kuu la Mwanza, Debora Nkungu alisema kwa bei ya rejareja nyanya kubwa moja wanauza Sh300 na za kawaida, tatu wanauza kwa Sh500.

Wilayani Ngara nyanya kilo moja ni Sh1,200 hadi Sh1,500 katika maeneo mengi yenye masoko ikiwamo miji ya Rulenge, Benako na Kabanga.

Wilayani Serengeti, fungu moja la nyanya nne limepanda kutoka Sh200 hadi Sh500.

Ndoo ndogo ya lita kumi ya nyanya inauzwa Sh10,000 kutoka Sh8,000 huku kubwa ikiuzwa kwa Sh20,000 badala ya Sh15,000.

Wilayani Tarime, fungu moja la nyanya la nne linauzwa Sh500 kutoka Sh200.

Mkulima wa nyanya wilayani Musoma Mkoa wa Mara, Mwita Matiko alisema kasha moja la nyanya linauzwa Sh50,000 kwa bei ya shambani huku mitaani likiuzwa kwa Sh60,000 hadi Sh70,000.

Alisema mwezi mmoja uliopita kasha moja lilikuwa likiuzwa Sh20,000 kwa bei ya shambani na Sh30,000 hadi 40,000 kwa bei ya mtaani.

Kilimanjaro

Mjini Moshi bei ya nyanya nayo imepanda ambako kasha moja linauzwa Sh65,000 hadi 70,000.

Mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Mbuyuni, Asha Rasul alisema nyanya zimeadimika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Rasul alisema kasha la nyanya linauzwa kwa Sh65,000 huku sado moja likiuzwa kati ya Sh6,000 na Sh8,000.

Alisema nyanya tatu zinauzwa kwa Sh500 na nyanya tano Sh1,000.

Musa Ally ambaye ni mfanyabiashara katika Soko la Kati alisema wananunua kasha moja la nyanya kwa Sh70,000 hadi Sh75,000 huku sado moja ikiwa Sh10,000.

Arusha na Manyara

Mkoani Arusha na Manyara nyanya zimepanda katika maeneo mbalimbali huku sado moja iliyokuwa ikiuzwa Sh3,000 awali, sasa inauzwa Sh10,000.

Mfanyabiashara Jane Minja wa Soko Kuu la Arusha alisema wamekuwa wakipata shida kupata nyanya na vitunguu kwa sasa.

“Mimi nauza sado ya nyanya kwa Sh8,000 na vitunguu ambavyo havipatikani kwa urahisi Sh10,000,” alisema Minja.

Akizungumzia hilo, Epimack Kaaya ambaye ni mfanyabiashara wa Soko la Tengeru Arusha alisema bei ya nyanya imepanda kwa kuwa mavuno yamepungua mwaka huu.

Mfanyabiashara wa Soko la Haydom, wilayani Mbulu Mkoa wa Manyara, Mariam Hamis alisema sado moja ya nyanya ni Sh5,000.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Happy Kayumbo alisema fungu la nyanya tatu au nne ndogo ni Sh500 na sehemu nyingine nyanya moja ndogo wanauza Sh100.

Imeandikwa na Kalunde Jamal (Dar), Julieth Ngarabali (Pwani) Johari Shani, Sada Amir na Saddam Sadick (Mwanza), Beldina Nyakeke (Musoma) Dinna Maningo (Tarime), Antony Mayunga (Serengeti), Shabani Ndyamkama (Ngara) na Janeth Joseph (Moshi)