Beka Fleva afunguka kifo cha Yamoto Band

Muktasari:

Aliyekuwa Meneja wa kundi hilo, Said Fella ’Mkubwa Fella’ alitaja sababu za kuvunjika


Nasra Abdallah, Mwananchi

Mei mwaka jana Kundi la muziki la Yamoto lilisambaratika rasmi na wasanii waliokuwa wakiunda kundi hilo walianza kufanya kazi kila mtu kivyake.

Wasanii waliokuwa wakiunda Yamoto ni pamoja na Dogo Aslay, Enock Bella, Beka na Maromboso ambapo karibu kila mmoja kwa sasa anapambania soko lake la muziki huku Dogo Aslay akiongoza kwa kutoa nyimbo nyingi zaidi.

Aliyekuwa Meneja wa kundi hilo, Said Fella ’Mkubwa Fella’ alitaja sababu za kuvunjika kuwa ni soko la muziki kushuka ambapo ilifika mahali mpaka wanatakiwa kufanya shoo kwa kiingilio cha kinywaji, jambo ambalo hakuwa tayari kulifanya kwa vijana wake hao.

Kutokana na hilo, anasema ndipo alipowakalisha chini na kuwashauri kuwa ni wakati sasa kila mmoja akatoka kivyake ili kuweza kuendeleza vipaji vyao na kujipatia kipato kitakachoweza kuendesha maisha yao ya kila siku.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti wakihojiwa wasanii hao kila mmoja amekuwa akielezea namna maisha yalivyo kwake kwa sasa baada ya kuvunjika kwa kundi hilo, ambapo wapo waliolimisi kutokana na namna walivyokuwa wakiishi kama familia. Mmojawapo ni Enock Bella ambapo siku za karibuni katika mahojiano yake na gazeti la Mwananchi, alisema alifikia hatua ya kurushiwa matusi na mashabiki kwamba alikuwa hana kipaji kwa kile walichodai wenzake walikuwa wakimbeba, jambo lililomuumiza hadi kupambana kurudi sokoni.

Wakati kwa upande wa Mbosso ambaye kwa sasa yupo chini ya lebo ya WCB, anasema kama sio bosi wa lebo hiyo, Diamond Platnumz kumuokoa alitaka kurudi kijijini baada ya kuona ndio mwisho wake wa kufanya kazi za muziki.

Kwa upande wa Dogo Aslay anasema anachoona anakimisi katika kundi hilo ni kwamba kwa sasa anapambana kutaka kila mtu ampende yeye na hata inapotokea lawama kwa sasa inabidi azibebe mwenyewe na sio kama bendi kama alivyokuwa na wenzake, jambo ambalo anakiri ni gumu kulilinda.

Wakati wasanii hao watatu wakieleza hayo, kwa upande wa Beka Fleva mkali wa kibao cha Nibebe, Sikinai, kibente na unanimaliza, yeye ametoa kauli tofauti kwamba hana anachokimisi katika kundi hilo.

Kwa nini hana anachokimisi

Akifafanua kwa nini hana anachokimisi katika kundi hilo hata kama limeshavunjika, Beka anasema ni kutokana na kwamba mapambano yake katika soko la muziki yanaendelea kama kawaida.

“Unajua nilipokuwa Yamoto japo tulikuwa wengi lakini nilijitahidi kupambana nami nionyeshe kipaji changu kwa Watanzania jambo ambalo naliendeleza hadi leo,”.

Kwani baada ya kusambaratika nilihakikisha watu wananielewa kwamba hata bila bendi mimi naweza na ninashukuru muziki wangu umeshajulikana nchini na kwa kiasi fulani nje ya nchi,”anasema.

Ni kutokana na hilo anasema tayari ameanza kupigiwa simu na baadhi ya wasanii wa nchi mbalimbali wakitaka kufanya naye kazi.

Pamoja na hilo, anasema kamwe hawezi kupadharau nyumbani kwani ndipo pamemfanya ajulikane na kuongeza kuwa huwezi kukubalika nje ya nchi yako kama watu wa nchini kwako hawakubali.

Katika matarajio yake anasema ni kufikia mafanikio waliyo nayo baadhi ya wasanii wa hapa Bongo na kuwataja baadhi yao kuwa ni pamoja na Ali Kiba, Diamond, Vanessa Mdee na Weusi.

Wito wake kwa wasanii wanaochipukia ni kuheshimu kazi yao na mashabiki wakati wote kwa kuwa bila wao si lolote katika Sanaa.

Wakati kwa wale ambao tayari wana mafanikio amewaomba wasiwe wazito kuwainua hawa wanaochipukia kwa kuwa hata wao walianzia huko na kushikwa mkono na baadhi ya watu hata kama sio wanamuziki.

Kwa upande wa serikali ameitaka kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuuza kazi zao na kufaidika na jasho lao na kuondoa sheria ambazo zimekuwa kikwazo kwao katika sanaa ukizingatia wengi wanapambana kivyaovyao hadi kufikia mafanikio.