Benki ya Dunia yamhakikishia Rais Magufuli fedha za barabara, reli

Muktasari:

Bird alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam jana na kubainisha maeneo ya kipaumbele kuwa ni miundombinu hususan barabara na reli, kuongeza uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na elimu kwa kujielekeza katika ubora na kuhakikisha idadi ya wanaoipata inaongezeka. Maeneo mengine ni kuboresha sekta ya afya, upatikanaji wa maji, usimamizi bora wa ardhi, mawasiliano, huduma za fedha jumuishi, vituo vya pamoja vya Serikali na kusaidia familia maskini.

       Dar es Salaam. Mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB) katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird amemhakikishia Rais John Magufuli kuwa imejipanga kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa miradi ya maendeleo hapa nchini ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Bird alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam jana na kubainisha maeneo ya kipaumbele kuwa ni miundombinu hususan barabara na reli, kuongeza uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na elimu kwa kujielekeza katika ubora na kuhakikisha idadi ya wanaoipata inaongezeka. Maeneo mengine ni kuboresha sekta ya afya, upatikanaji wa maji, usimamizi bora wa ardhi, mawasiliano, huduma za fedha jumuishi, vituo vya pamoja vya Serikali na kusaidia familia maskini.

Mwakilishi huyo wa Benki ya Dunia alimpongeza Rais Magufuli kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na benki hiyo.

“Mwaka uliopita Benki ya Dunia imetoa mikopo nafuu yenye thamani ya Dola 1.2 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh2.7 trilioni) kwa Tanzania, fedha hizi zimekwenda katika miradi mbalimbali na tunafurahi kuwa miradi hiyo inakwenda vizuri na wananchi wanafurahia,” alisema.

“Kwa sasa tunapanga namna tutakavyotoa mikopo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo katika kipindi kijacho.”

Kwa upande wake, Rais Magufuli aliishukuru benki hiyo kwa ushirikiano wake na Tanzania katika maendeleo na alimhakikishia Bird kuwa Serikali itazisimamia vizuri fedha zote zinazotolewa na benki hiyo ili zilete matokeo yanayotarajiwa.

Rais alisema maeneo ambayo benki hiyo imeyataja kuwa kipaumbele katika fedha zitakazotolewa kuanzia sasa ni muhimu kwa ustawi wa Tanzania.

Alisisitiza kuwa fedha zitakazotolewa kama mkopo zitaelekezwa katika maendeleo na si vinginevyo. “Naishukuru sana Benki ya Dunia kwa kutuunga mkono, nitafurahi kuona mnaendelea kutupatia fedha ambazo zinaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na kuleta manufaa mapana na endelevu, badala ya kugawa fedha kwa watu na baadaye nchi inakuja kuzilipa kwa kukusanya kodi za wananchi,” alisema.