Benki ya Posta yapata faida ya mabilioni

Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi.

Muktasari:

Benki ya Posta Tanzania (TPB) imetangaza kupata faida ya Sh8.84 bilioni kabla ya kukatwa kodi kwa kipindi cha miezi sita, ikilinganishwa na Sh5.48 bilioni zilizopatikana mwaka 2015 sawa na ukuaji wa asilimia  61.47.

Dar es Salaam. Benki ya Posta Tanzania (TPB) imetangaza kupata faida ya Sh8.84 bilioni kabla ya kukatwa kodi kwa kipindi cha miezi sita, ikilinganishwa na Sh5.48 bilioni zilizopatikana mwaka 2015 sawa na ukuaji wa asilimia  61.47.

Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi amewaambia waandishi wa habari leo kwamba ukuaji huo wa faida umewezesha kukua kwa mtaji wa wawekezaji hadi kufikia Sh48 bilioni kutoka Sh37 bilioni Juni, 2015.

“Mapato ya benki kwa nusu mwaka 2016 yaliongezeka hadi kufikia Sh42.5 bilioni kutoka Sh34 bilioni iliyofikiwa nusu ya mwaka 2015, huu ni ukuaji wa asilimia 38,” alisema Moshingi.

Alisema katika kipindi hichohicho, amana za wateja ziliongezeka na kufikia Sh294.64 bilioni kutoka Sh263.68 Juni mwaka 2015 sawa na ukuaji wa asilimia 11.74.

“Mikopo imeongezeka kufikia Sh278 bilioni kutoka Sh241.51 bilioniJuni, 2015 sawa na ongezeko la asilimia 15.22. sehemu kubwa ya mikopo imetolewa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo pamoja na wafanyakazi wa sekta ya umma na Serikali kuu,” alisema Moshingi.

Aliongeza kuwa rasilimali za benki zilikua hadi kufikia Sh390.8 bilioni kutoka Sh333.96 bilioni Juni 2015 ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.16.

Mbali na mapato hayo, Moshingi aliendelea kutaja mafanikio mengine ikiwa pamoja na ujenzi wa tawi la benki hiyo lililopo Songea mkoani Ruvuma lililofunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na jingine la Babati Mkoani Manyara lililofunguliwa na Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru mwaka huu.

“Matawi hayo yamejengwa kwenye viwanja vinavyomilikiwa na TPB. Benki ilihamishia makao makuu yake makuu kutoka jengo la Extelecoms lililopo mtaa wa Samora na kuhamia kwenye jengo la Millenium Towers Kijitonyama,” alisema.

Pamoja na mafanikio hayo, Moshingi alisema TPB itaendelea kutoa mikopo kwa vikundi vidogo, kushirikiana na Baraza la Uwezesheji wananchi kiuchumi NEEC) kuinua uchumi wa vikundi hivyo na kufungua vikundi visivyo rasmi ambapo hadi sasa wamefungua akaunti 30.