Biashara nyumba za kupanga Moshi yaporomoka

Muktasari:

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini hata baadhi ya wenye nyumba waliokuwa wakitoza kodi ya pango kwa fedha ya Marekani sasa wanalazimika kutoza kwa Shilingi ya Tanzania.

Moshi. Soko la nyumba za kupanga hususan eneo la Shanty Town mjini Moshi linalokaliwa na vigogo wengi limeporomoka ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini hata baadhi ya wenye nyumba waliokuwa wakitoza kodi ya pango kwa fedha ya Marekani sasa wanalazimika kutoza kwa Shilingi ya Tanzania.

Mbali na kuporomoka kwa kiwango cha kodi ya pango pia, baadhi ya wafanyabiashara wenye fremu za maduka, nao wana mpango wa kuzirejesha kwa wamiliki kwa madai kuwa biashara imekuwa ngumu.

Maeneo ya Shanty Town, baadhi ya nyumba zilikuwa zikikodishwa kwa Dola 400 za Marekani (takriban Sh800,000) hadi Dola 800 (Sh1.6 milioni) kwa mwezi, kuanzia mwishoni mwa mwaka jana zimeanza kukosa wapangaji.

Kiwango hicho ni sawa na kati ya Sh880,000 na Sh1.7 milioni za Tanzania kwa kiwango cha ubadilishaji fedha cha Dola moja ya Marekani kwa Sh2,200 za Tanzania.

“Kuna nyumba hapa (Shanty) inakodishwa kwa Dola 800 mpaka leo haijapata mpangaji baada ya mpangaji wa awali kuondoka. Kwa maisha gani ya sasa mtu alipe hizo hela?” kilidokeza chanzo chetu na kuongeza:

“Wengine walikuwa wakikodisha kwa nyodo, anakuambia kama hutaki pita, lakini sasa wanabembeleza na wanapokea hata kwa shilingi.”

Mmoja wa madalali ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema nyumba katika eneo la Soweto zilizokuwa zikikodishwa kati ya Sh300,000 na Sh400,000 kwa mwezi, kodi yake imeshuka pia.

“Mpangaji akishamaliza mkataba wake wanajikuta kila anayetaka kupangisha haafiki hiyo kodi inabidi mjadiliane. Sasa hivi zinaanzia Sh150,000 hadi Sh250,000,” alisema.

Mfanyabiashara wa mjini Moshi, Justine Minja alisema hali ya biashara siyo nzuri na baadhi ya waliokodi fremu za maduka wanafikiria kuzirejesha maana kiwango cha biashara kimeshuka.

“Zamani kupata hizi fremu huku Double Road (Barabara ya Mawenzi) watu walikuwa lazima watoe kilemba (cha juu) tena mamilioni lakini sasa hivi hakuna hiyo,” alisema Minja.

Meya wa Manispaa ya Moshi ambaye anaishi eneo la Shanty Town, Raymond Mboya alipoulizwa jana alikiri baadhi ya wamiliki wa nyumba wa eneo hilo kukosa wateja na kulazimika kushusha kodi.

Mboya alisema hofu aliyonayo ni hatua ya wafanyabiashara wenye maduka kutaka kufunga biashara.

Alisema hatua hiyo itasababisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Halmashauri kuathirika kimapato.

“Hakuna mazingira mazuri ya biashara, haiwezekani wewe mwenye duka unauza sufuria na nje kuna Machinga naye anauza bidhaa hiyo tena bila kulipa kodi,” alisema Mboya.

Alitoa rai kwa Rais John Magufuli na wawakilishi wake mikoani, kutafuta njia ya kufafanua kauli yake iliyorejesha wimbi kubwa la machinga katika maeneo yasiyoruhusiwa. Alisema hali hiyo inaathari kubwa kiuchumi.

Hivi karibuni mfanyabiashara mashuhuri, Philemon Ndesamburo aliwatahadharisha wenzake mjini Moshi, kukopa fedha benki kwa tahadhari akisema upepo wa biashara umebadilika tangu mwaka jana.

Ndesamburo alisema baadhi ya wafanyabiashara waliokopa fedha kwenye taasisi za kifedha na kuzitumbukiza kwenye biashara zao wamejikuta kwenye wakati mgumu baada ya biashara zao kuyumba na kushindwa kurejesha mikopo yao kwa wakati.

“Lazima tuchukue tahadahri kubwa, hali siyo shwari kama tunavyodhania, tusije tukajikuta tunafilisiwa na benki,” alisema.