Tira yaandaa waraka kuimarisha biashara ya bima

Muktasari:

Waraka huo unaotarajiwa kuanza kutumika Januari Mosi,2018 unatoa masharti ya biashara kwa kampuni za bima mtawanyo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), imeandaa waraka utakaosaidia kuongeza ukubwa wa biashara na kuimarisha ustawi wa kampuni za ndani.

Hatua hiyo inalenga kupunguza kampuni za nje kutawala biashara ya bima nchini.

Waraka huo unaotarajiwa kuanza kutumika Januari Mosi,2018 unatoa masharti ya biashara kwa kampuni za bima mtawanyo (reinsurance) na madalali wa mtawanyo kutoka nje ya nchi.

Katika uzinduzi wa waraka huo leo Jumatatu Desemba 11,2017 Kamishna wa Bima, Dk Baghayo Saqware amesema utaratibu wa kupeleka biashara za bima nje ya nchi ni suala la kawaida duniani na utaratibu huo unapofanyika vizuri huleta faida kwa soko la ndani lakini utaratibu usipokuwa mzuri matokeo yake huwa hasi.

Ameyataja maeneo yenye upungufu katika biashara ya bima mtawanyo kuwa ni matumizi ya kupindukia ya bima hiyo kwa njia ya makubaliano hata sehemu zinazohitaji mkataba, kupeleka biashara ya bima nje kwa asilimia 100, ushiriki hafifu wa kampuni za ndani katika kutoa bima za majanga makubwa na kampuni za ndani kutoa upendeleo kwa kushirikisha kampuni za nje zaidi kuliko za ndani.

Mwingine amesema ni kampuni za ndani kufanya biashara na kampuni za nje zisizo na viwango, kukosekana kwa uwazi katika biashara hiyo na baadhi ya kampuni kupeleka nje biashara ambazo muda wake umeisha.

Makamu mwenyekiti wa chama cha kampuni za bima nchini, Charles Sumbwe amesema waraka huo ni matokeo ya mapendekezo ya wadau kuhusu namna ya kuboresha biashara hiyo nchini.