Biashara ya karafuu Zanzibar kuendelea kudhibitiwa

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mwendeshaji wa shirika hilo, Dk Said Seif Mzee alisema hayo ofisini kwake alipozungumza na gazeti hili kutokana na kuwapo taarifa za wananchi kudai zao hilo ni vema lisimamiwe na kampuni binafsi ili kutoa fursa zaidi ya kipato kwa wakulima.
  • Alisema shirika hilo halitatoa zao hilo ndani ya usimamizi wa Serikali kwa kuwa linawaongezea kipato.

Zanzibar. Shirika la Biashara la Karafuu Zanzibar (ZSTC) limesema halina nia ya kulibinafsisha zao hilo kwa kampuni au watu binafsi kutokana na kuwa tegemeo kwa Serikali.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa shirika hilo, Dk Said Seif Mzee alisema hayo ofisini kwake alipozungumza na gazeti hili kutokana na kuwapo taarifa za wananchi kudai zao hilo ni vema lisimamiwe na kampuni binafsi ili kutoa fursa zaidi ya kipato kwa wakulima.

Alisema shirika hilo halitatoa zao hilo ndani ya usimamizi wa Serikali kwa kuwa linawaongezea kipato.

Dk Said alisema uamuzi huo unatokana na msimamo wa Baraza la Mapinduzi visiwani humo chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, kueleza kuwa hakuna sababu ya karafuu kusimamiwa nje ya shirika la Serikali.

Mkurugenzi huyo alisema Serikali inalenga kuliimarisha zao hilo kwa masilahi ya wananchi na Taifa, hivyo dhana ya kuwapo ubinafsishaji haina nafasi.

Ili kuimarisha kilimo cha karafuu alisema mikakati iliyopo ni kugawa bure miche ya mikarafuu, kutoa mafunzo kwa wakulima na kuongeza bei ya zao hilo.

Alisema awali bei ya kununua karafuu kutoka kwa mkulima ilikuwa Sh5,000 kwa kilo, lakini sasa ni Sh14,000 kiwango ambacho ni sawa na asilimia 80 ya mauzo ya soko kuu la biashara nje ya nchi.

Mkurugenzi huyo alisema shirika limejipanga kwa kuweka mikakati madhubuti ya ulinzi wa karafuu dhidi ya utoroshwaji na uuzaji wa magendo nje ya nchi.

Aliongeza kuwa kipo kikosi kazi maalumu kinachojumuisha wakuu wa mikoa na wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hata hivyo, baadhi ya wakulima walisema masilahi yao yanahitaji kuboreshwa zaidi.

Mkulima mkazi wa Donge, Kaskazini Unguja, Hamad Said alisema hawezi kushindana na Serikali kwa kutouza zao hilo kwa shirika lao, ila ni vema kuangalia ugumu wa kilimo cha karafuu ili uendane na bei ya ununuzi.

Alisema wanaamini wazi kuwa bei ya nje ya nchi ni kubwa ndiyo maana kuna watu bado wanaonekana kufanya magendo, hivyo ni wakati mzuri kwa Serikali kushirikiana na wakulima ili kuwapa moyo zaidi wa kilimo hicho.

Sheha wa Kilindi, Kaskazini Unguja, Ali Omar Mussa alisema wakulima wamepata mafanikio kupitia kilimo cha karafuu, lakini inahitajika nguvu ya pamoja ili kufikia malengo waliyokusudia.